Habari za Kitaifa

Sakaja katika kinywa cha mamba Raila akiendeleza mikakati ya kumwokoa

Na COLLINS OMULO, KEVIN CHERUIYOT September 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga jana alishindwa kumwokoa Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja baada ya madiwani wa Nairobi kumkaidi na kuapa kukamilisha mipango ya kumng’oa kiongozi huyo madarakani.

Jana, Bw Odinga alikutana na uongozi wa Bunge la Kaunti, mkutano ambao ulikuwa wa pili ndani ya siku nne.

Mkutano huo ulikuwa wa kuwarai wawashawishi wenzao waachane na mpango wa kumng’atua gavana huyo enzini.

Idadi ya madiwani ambao wanataka Bw Sakaja atimuliwe nayo inaendelea kuongezeka na kufikia jana walikuwa 85 kutoka 70 mnamo Ijumaa wiki jana.

Juhudi za kusitisha mchakato huo zinaonekana kugonga mwamba.

Bunge la Kaunti ya Nairobi kwa sasa liko likizoni kwa muda wa mwezi mmoja baada ya kuanza likizo Agosti 7 ambayo itadumu hadi Septemba 23.

Mnamo Ijumaa, kulikuwa na mkutano uliojaa hisia tele katika makazi ya Bw Odinga mtaani Karen, Nairobi, ambao ulihudhuriwa na Bw Sakaja na uongozi wa Bunge la Kaunti.

Duru zinaarifu kuwa mkutano huo ulioanza saa nne mchana, uliendelea hadi jioni lakini hakuna suluhu iliyoafikiwa.

Ilidokezwa kwamba Bw Odinga alimuunga mkono Bw Sakaja na kumwambia azingatie utoaji wa huduma kwa raia na kutimiza ahadi zake na kutoa pesa za basari na maendeleo kwa wadi mbalimbali.

Bw Odinga pia alimwahidi Bw Sakaja kuwa angezungumza na viongozi wengine wa Bunge la Kaunti wiki hii ili kumwokoa.

Hapo jana, Bw Odinga alikuwa na mkutano mwingine wa kumwokoa gavana huyo katika afisi za wakfu wa Jaramogi Oginga Odinga, Nairobi.

Mkutano huo uliojaa hisia na majibizano makali pia ulihudhuriwa na Bw Odinga, Kiongozi wa Wengi Nairobi, Peter Imwatok, Spika Ken Ng’ondi, Kiongozi wa Wengi Moses Ogeto na Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Bajeti Wilfred Odalo.

Uongozi huo wa Kaunti ulikashifiwa kwa kunufaika na ‘wema’ wa Bw Sakaja kisha kukosa kusikia kilio cha madiwani.

Hakuna chochote kilichoafikiwa katikamkutano huo huku waliohudhuria wakidai walikuwa katika shinikizo za kumtimua Bw Sakaja kutokana na jinsi hali ilivyo kiuongozi katika Kaunti ya Nairobi.

Aliyekuwa Diwani wa South C, Osman Khalif ambaye kwa sasa anafanya kazi kwenye Afisi ya Gavana pia alihudhuria mkutano huo pamoja na Mkuu wa Wafanyakazi David Ndung’u Njoroge.

Wawili hao walikashifiwa kwa kuwazuia madiwani kumfikia Gavana.

“Tuna mkutano mwingine bila Raila baada ya chakula cha mchana kisha Jumanne (leo) tutakutana na Raila,” kidokezo kikasema.

Aidha, mbunge mmoja kutoka Kaunti ya Nairobi aliyekuwa akifuatilia mkutano huo aliambia Taifa Leo kuwa leo uongozi wa Kaunti utawasilisha ripoti yake kwa Raila ambapo hatima ya gavana huyo itaamuliwa.

“Ripoti hiyo ndiyo itaamua mustakabali wake, hapo ndipo tutajua kama atanusurika au mpango wa kumng’atua utaendelea mbele,” akasema mbunge huyo.

Kufikia jana usiku, wakati wa kuchapisha habari hizi, mkutano kati ya uongozi wa Kaunti na baadhi ya madiwani ulikuwa bado unaendelea.

Inadaiwa Ijumaa iliyopita, Bw Sakaja alimtafuta mwanasiasa mkongwe wa Nairobi mwenye usuli Mlima Kenya amshawishi mbunge mmoja rafiki mkubwa wa Raila.

Mbunge huyo alitwikwa jukumu la kuwasilisha kilio cha Bw Sakaja kwa Raila.

Kwa mujibu wa sheria za Bunge la Kaunti ni thuluthi tu ya saini inayohitajika ndipo hoja ya kumng’atua gavana mamlakani.

Idadi hiyo ni saini 41 kati ya madiwani 123 ikizingatiwa diwani mmoja, Joel Muneve ambaye alikuwa diwani wa Kariobangi Kaskazini alifariki mnamo Aprili.

Hata hivyo, notisi ya kuitisha kikao cha kujadili hoja ya kumtimua gavana lazima itoke kwa Spika baada ya kupokea mawasiliano kutoka kwa afisi ya upande wa Wengi au Wachache.

Madiwani mbalimbali waliohojiwa walisema kuwa safari ya Bw Sakaja imefikia mwisho na wako tayari kumng’atua.

Baadhi ya madiwani walioongea na Taifa Leo na kusema wako radhi kuhakikisha Bw Sakaja anaenda nyumbani ni Naibu Kiongozi wa Wachache Waithira Chege, Robert Alai (Kileleshwa), Sospeter Mumbi (Roysambu), Maurice Ochieng’ (Mountain View) na Geoffrey Majiwa (Baba Dogo) miongoni mwa wengine.