Kimataifa

Maporomoko ya ardhi yaua 1,000 Sudan, kijiji chabaki mtu mmoja tu

Na MASHIRIKA, BENSON MATHEKA September 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TAKRIBAN watu 1,000 wamefariki dunia kutokana na maporomoko ya ardhi katika Milima ya Marra, magharibi mwa Sudan, kwa mujibu wa kundi la waasi la Sudan Liberation Movement/Army (SLM/A).

Kulingana na taarifa ya kundi hilo, mvua kubwa iliyonyesha kwa siku kadhaa ilisababisha maporomoko hayo siku ya Jumapili, na kusababisha kijiji cha Tarasin kusombwa kabisa, kikisalia na mtu mmoja tu aliyeokoka.

Kundi hilo limeomba msaada wa kibinadamu kutoka kwa Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kikanda na kimataifa, likisema kuwa hali ni ya dharura.

Wakazi wengi wa jimbo la Darfur Kaskazini walikuwa wamekimbilia Milima ya Marra kutafuta hifadhi, baada ya vita kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF) kuwafurusha kutoka makwao.

Gavana wa Darfur anayeegemea upande wa jeshi, Minni Minnawi, aliitaja ajali hiyo kama “janga la kibinadamu.”

“Tunaomba mashirika ya misaada ya kimataifa kuingilia kati haraka na kutoa msaada katika wakati huu mgumu, kwa sababu janga hili ni kubwa kuliko uwezo wa watu wetu kulimudu,” alisema kupitia taarifa iliyonukuliwa na shirika la habari la AFP.

Picha kutoka eneo la tukio zinaonyesha mito miwili mikubwa ya maji yaliyojaa udongo kwenye mlima, iliyoungana katika sehemu ya chini ambapo kijiji cha Tarasin kilikuwa kimejengwa.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka Aprili 2023 kati ya jeshi la Sudan na RSF vimeitumbukiza nchi hiyo katika baa la njaa na vimesababisha tuhuma za mauaji ya halaiki katika eneo la Darfur.

Takwimu kuhusu idadi ya waliouawa katika vita hivyo zinatofautiana kwa kiasi kikubwa, lakini afisa mmoja wa Amerika alikadiria kuwa hadi watu 150,000 wameuawa tangu mapigano yaanze mwaka 2023.

Takriban watu milioni 12 wamehama makazi yao.

Kundi la Sudan Liberation Movement/Army linalodhibiti eneo lililoathirika na maporomoko hayo ya ardhi yameapa kushirikiana na jeshi la Sudan kupambana na RSF.

Wakazi wengi wa Darfur wanaamini kuwa RSF na wanamgambo washirika wao wameanzisha vita vya kikabila kwa lengo la kubadilisha eneo hilo lenye mchanganyiko wa makabila kuwa chini ya utawala wa Waarabu pekee.