Afisa wa Kenya aliyefia Haiti atambuliwa kama Koplo Kennedy Mutuku Nzuve
AFISA Mkenya aliyefariki katika ajali ya barabarani akiwa kwenye doria chini ya kikosi cha kulinda amani Haiti (MSS) ametambuliwa kama Koplo Kennedy Mutuku Nzuve.
Bw Mutuku na raia wawili walifariki Jumapili baada ya ajali iliyohusisha magari mawili ya kivita katika barabara ya Kenscoff–Pétion-Ville jijini Port-au-Prince, mji mkuu wa Haiti.
Ajali ilitokea wakati wa shughuli ya uokoaji iliyohusisha magari mawili ya MaxxPro. Gari moja lilikuwa linaburuta lingine na katika hali hiyo, moja lilipata hitilafu za kimitambo na kusababisha ajali,” taarifa ya MSS ikasema.
Ukosefu wa vituo vya matibabu ya hali ya juu humaanisha kwamba maafisa waliojeruhiwa wanasafirishwa hadi Jamhuri ya Dominican kwa matibabu.
“Maafisa watatu waliojeruhiwa vibaya wamepelekwa Jamhuri ya Dominican kwa matibabu spesheli, wengine wanapokea matibabu katika hospitali ya Aspen,” msemaji wa MSS Jack Ombaka akasema.
Bw Mutuku, mzaliwa wa Kaunti ya Machakos alikuwa na umri wa miaka 41.
Alitumikia vitengo mbalimbali ikiwemo Rapid Deployment Unit (RDU).
Alitumwa maeneo ya Narok, Baringo kabla ya kujumuishwa kwenye kikosi cha kwenda Haiti.
Kifo cha Mutuku kinaongeza idadi ya maafisa waliopoteza maisha yao wakiwa Haiti kufikia watatu tangu kikosi hicho kitumwe taifa hilo la Caribbean mwaka jana.
Mnamo Februari, Konstebo Samuel Tompoi Kaetuwai alifariki baada ya kupigwa risasi na magenge wakati wa operesheni.
Mwezi mmoja baadaye, Benedict Kabiru Kuria, afisa mwingine Mkenya alivamiwa na kuuawa na genge eneo la Artinobinte.