Dimba

Berlin Marathon 2025 kuruhusu washiriki kusikiliza muziki wakitimka

Na GEOFFREY ANENE September 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WANARIADHA wataruhusiwa kusikiliza muziki katika Berlin Marathon kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano hayo hapo Septemba 21, 2025.

Duru hiyo ya tano ya Marathon Kuu Duniani (WMM) imetangaza kuwa washiriki watakubaliwa kutumia visikizi, hatua inayokomesha marufuku ya miongo mingi ambayo ilikuwa hairuhusu wakimbiaji kuvaa vifaa vya kusikilizia sauti.

Uamuzi wa waandalizi wa Berlin Marathon unaakisi mtindo wa kimataifa unaokua unaolenga kuleta usalama, ujumuishi na kuboresha furaha ya wakimbiaji. Teknolojia ya visikizi inawawezesha wanariadha kusikia muziki wao, huku wakibaki na uwezo wa kusikia mazingira yao, jambo linalopunguza hofu za kiusalama na kuongeza hamasa siku ya mashindano.

Berlin Marathon huvutia zaidi ya wakimbiaji 50,000 kila mwaka. Inajulikana kwa njia yake tambarare na ya kasi ambayo imeshuhudia rekodi 13 za dunia, na kuongeza hadhi yake duniani.

Mkurugenzi wa Mashindano, Mark Milde, alisema kuwa mabadiliko hayo ni “faida kwa pande zote,” akibainisha kuwa wakimbiaji wengi tayari hujizoesha na visikizi, hivyo kuruhusiwa rasmi kutawafanya wajisikie huru zaidi.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya SCC inayoandaa Berlin Marathon, Christian Jost, alitaja uamuzi huu kuwa hatua ya kihistoria. Alisisitiza kuwa muziki sasa ni sehemu muhimu ya utamaduni wa mbio.

Makala ya 2025 pia yamemteua Shokz, waanzilishi wa teknolojia ya visikizi, kuwa mshirika rasmi wa vifaa vya kusikilizia. Kwa mujibu wa Timo Gohler wa SCC, ushirikiano huu si udhamini pekee, bali pia unalenga kubadilisha na kuboresha uzoefu wa wakimbiaji.

Ingawa wanariadha wa kulipwa bado hawataruhusiwa kutumia visikizi kutokana na kanuni za kimataifa, ruhusa kwa wakimbiaji wa kawaida ni mabadiliko makubwa ya kitamaduni kwa marathon hiyo.

Waandalizi wamesisitiza kuwa usalama na umakini wa wakimbiaji bado ni kipaumbele cha juu. Baadhi ya watimkaji wa kulipwa kutoka Kenya watakaoshiriki ni bingwa wa Tokyo Marathon mwaka 2023 Rosemary Wanjiru, na mshindi wa London Marathon 2025 Sabastian Sawe.