Upinzani hauoni mazuri serikali imetekeleza, alalamika Rais Ruto
RAIS William Ruto amepuuzilia mbali madai ya viongozi wa upinzani kuhusu gharama ya juu ya maisha, huku akitetea sera za kiuchumi za serikali yake.
Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa Maonyesho ya Kimataifa ya Mombasa katika uwanja wa Mkomani, Rais alisema serikali imefanikiwa kupunguza gharama ya chakula na inaendelea kujenga uchumi unaowanufaisha Wakenya wote.
Akiwashutumu wakosoaji wake, Rais aliwataka Wakenya kujikita katika uzalendo, ujasiri, maono pana, na uongozi wenye ujasiri unaoangalia ustawi wa muda mrefu wa taifa badala ya kujihusisha na siasa za uchaguzi ujao.
“Tungeweza kuchukua njia rahisi, kujikita katika maeneo machache na kuahirisha mengine kama vile wakosoaji walivyosema kuwa ajenda yetu haiwezi kufanikishwa. Lakini tulikataa njia rahisi. Tulichagua njia sahihi kwa sababu ndiyo njia ya kuelekea kwa Kenya bora,” alisema Rais Ruto.
Aliahidi kuwa serikali yake itaendelea kuwekeza katika maeneo muhimu hadi kila sekta iakisi ahadi ya mabadiliko aliyotoa kwa wananchi.
“Ni lazima tukatae kuvunjwa moyo na wale wasioamini mafanikio. Manabii wa uharibifu wanaoona ubaya pekee na kuisema vibaya nchi yetu hawapaswi kufaulu. Sisi ndio kizazi kinachopaswa kuweka malengo makubwa na ya ujasiri,” akaongeza.
Rais Ruto alisisitiza kuwa hataacha kualika makundi mbalimbali katika Ikulu ya Nairobi licha ya ukosoaji kwamba taasisi hiyo inapoteza hadhi.
“Ikulu ni ya wananchi. Tutaendelea kufanya serikali iwe ya watu. Serikali kuu na Bunge zitakuwa wazi kwa wananchi kwa sababu wao ndio wamiliki wa taasisi hizi kupitia Katiba,” alieleza Rais.
Kuhusu kilimo, Rais alisema sekta hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi kwa miongo kadhaa licha ya kuwa nguzo kuu ya uchumi wa taifa.
Alitaja matatizo hayo kama hasara baada ya mavuno, kutegemea mvua, wadudu na magonjwa kama baadhi ya changamoto ambazo wakulima wamekuwa wakikumbana nazo, lakini hali imeanza kubadilika.