Habari za Kitaifa

IEBC hatimaye yarejesha usajili wa wapigakura Gen Z wakiambiwa kipenga kimepulizwa

Na MOSES NYAMORI September 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) imepuliza kipenga kuelekea uchaguzi mkuu ujao huku ikitarajiwa kuanza kuwasajili wapigakura mwishoni mwa mwezi huu.

IEBC ilisema usajili wa wapigakura utaanza rasmi Septemba 29, 2025.

Unalenga kuwasajili wapigakura wapya milioni 5.7.

Wapigakura ambao wanalengwa hasa ni vijana wa Gen Z ambao wamekuwa wakishiriki maandamano ya kupigania mageuzi nchini wakilalamikia pia ukosefu wa ajira.

Usajili wa wapigakura usiokuwa na kikomo ulisitishwa Januari mwaka jana kutokana na IEBC kutokuwa na makamishina wote.

Hii ni baada ya kustaafu kwa aliyekuwa Mwenyekiti Wafula Chebukati na baadhi ya makamishina mnamo Januari 2023.

Kwa mujibu wa IEBC, sajili ya sasa ya IEBC ina wapigakura milioni 22.1 na kwa kuwa inalenga wapigakura milioni tano zaidi, huenda kukawa na jumla ya wapigakura milioni 27.8 mnamo 2027.

“Tume inalenga wapigakura wapya milioni 5.7, wengi wao wakiwa vijana ambao wametinga umri wa kupiga kura,” ikasema IEBC kwenye tovuti yake.

“Kama sehemu ya maandalizi yake kwa uchaguzi wa 2027, tume inapanga kuchapisha vituo 55,393 vya upigaji kura kutoka 46,229 mnamo 2022,” ikaongeza.

IEBC pia itawasilisha zabuni ya kununua vifaa 46,229 vya kielektroniki (KIEMS) kwa Sh7 bilioni.

Vifaa hivyo vitachukua nafasi ya vile 45,352 ambavyo vinatumika kwa sasa na vilinunuliwa mnamo 2017.

IEBC imeanza shughuli ya kuwanasa wapigakura wapya kwa kuorodhesha maeneo ya usajili, kuthibitisha vituo vya sasa vya upigaji kura na vile ambavyo vimependekezwa maeneo mbalimbali nchini.

Pia, IEBC itakuwa ikiandaa uhamasisho kuanzia kiwango cha eneobunge ili kuwarai Wakenya wajisajili kama wapigakura.

Shughuli nyingine ni kupima ufaafu wa vifaa vya KIEMS, kuwapa mafunzo maafisa wa uchaguzi na pia wapigakura kuhusu umuhimu wa kushiriki uchaguzi.

“Shughuli hizi ni muhimu katika kuhakikisha kila Mkenya anashiriki uchaguzi na kuamua mustakabali wa uongozi wa taifa lake.

Hasa wanaolengwa ni wale ambao wametimiza umri wa miaka 18 na bado hawajisajili au hawajathibitisha maelezo yao kuhusu upigaji kura,” ikasema IEBC.

Tayari, kura za Gen Z zinawaniwa sana na mirengo yote ya kisiasa ambayo inalenga kushinda uchaguzi mkuu wa 2027.

Ingawa baadhi ya Gen Z walikuwa wametinga umri wa kupiga kura mnamo 2022, hawakushiriki uchaguzi kutokana na wengi wao kutomakinikia masuala ya uongozi.

Hata hivyo, changamoto za kimaisha ambazo zinawakabili pamoja na nchi, zimesababisha wazinduke na wamekuwa sura ya maandamano dhidi ya serikali ya Kenya Kwanza.

Tangu maandamano ambayo yalitikisa nchi na hata majengo ya bunge kuvamiwa ambapo mauaji yalishuhudiwa, Gen Z wamekuwa wakisema kuwa wanapigania uongozi bora wala hawajitambulishi na kabila lolote.

Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) lilitoa takwimu ambazo zinaonyesha kuwa zaidi ya Gen Z milioni 14 watakuwa radhi kupiga kura mnamo 2027.

Hii itasukuma mbele idadi ya vijana ambao wako tayari kupiga kura kwa asilimia 79.4.

Wakenya ambao watakuwa na umri wa kati ya miaka 18 hadi 34 watakuwa milioni 17.8, hii ikiashiria jukumu muhimu ambalo watatekeleza katika uchaguzi huo.

Katika uchaguzi mkuu wa 2022, Rais Ruto alishinda kwa kura 7,176,141 nayo Kinara wa ODM Raila Odinga akapata kura 6,942,930.

Sajili ya IEBC zinaonyesha kuwa wakati huo kulikuwa na wapigakura milioni 22.1 lakini milioni 14.3 pekee ndiyo walijitokeza na kushiriki kura hiyo.

Hii ina maana kuwa wapigakura milioni nane hawakushiriki uchaguzi huo.

Ripoti ya IEBC ilionyesha kuwa idadi ya vijana ambao walijitokeza kupiga kura 2022 ilikuwa chini.

Ripoti hiyo ilionyesha kuwa vijana waliojisajili kati ya miaka 18-34 walikuwa 8811,691 ambayo ni asilimia 40 ya jumla ya wapigakura.

Hii inaonyesha kuwa, idadi ya vijana ilikuwa tosha kubadilisha matokeo ya uchaguzi huo na kuamua mshindi wa urais.

“Gen Z watakuwa na usemi na kura zao zitaamua matokeo ya uchaguzi wa 2027,” akasema Mchanganuzi wa Masuala ya Kisiasa Javas Bigambo.

“Huwezi kuwapuuza vijana tena kwa sababu matukio ya kisiasa na maandamano yanaonyesha kuwa wana matamanio ya kushiriki mabadiliko ya uongozi 2027,” akaongeza.