Magavana wakurupuka kujilinda na wimbi la ‘timua timua’
HUKU hoja nyingi za kutaka kuondolewa kwa magavana zikiambulia patupu, maseneta sasa wameungana na magavana wakitaka mchakato wa kuwaondoa viongozi hao madarakani ushughulikiwe upya ili kuzuia matumizi mabaya ya hoja hizo.
Hii inajiri baada ya kesi kadhaa za kuondoa magavana kufeli kwa msingi wa kiutekelezaji katika Seneti.
Hali hii inatokea wakati ambapo hoja dhidi ya magavana na manaibu wao zimeongezeka, huku Seneti ikishughulikia angalau kesi nane za kuwaondoa viongozi hao wa kaunti tangu uchaguzi wa 2022.
Ingawa magavana wamewalaumu madiwani kwa kutumia mchakato wa kuondoa viongozi kama silaha ya kisiasa isiyo na msingi, maseneta sasa wanataka kuunda kanuni zitakazowaongoza madiwani wanapoandaa hoja hizo.
Tangu mwaka wa 2013, Seneti imeshughulikia takriban kesi 19 za kuondoa magavana, huku nane pekee zikiwa ndizo zimefaulu, na tatu zikisitishwa kabla ya kuanza kusikilizwa kikamilifu.
Hivi majuzi, Seneti ilichunguza hoja ya kumuondoa Gavana wa Kericho, Eric Mutai kwa mara ya pili ndani ya mwaka mmoja, huku hoja dhidi ya Gavana wa Isiolo, Abdi Guyo ikitupiliwa mbali mwezi uliopita kwa sababu za kiutekelezaji, madiwani wakishindwa kuthibitisha iwapo vikao vya kujadili hoja hiyo vilifanyika.
Hoja nyingi za kuondoa magavana zinalenga tuhuma za ufisadi, unyanyasaji na matumizi mabaya ya ofisi.
Hata hivyo, magavana wanaolaumiwa wanasema wanalengwa kisiasa na kunyanyaswa kimakusudi.
Jumanne, Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Ahmed Abdullahi alilalamikia matumizi mabaya ya hoja hizo, akisema nyingi zinachochewa na siasa, migawanyiko ya makundi, na mapambano ya urithi wa uongozi, badala ya kuwa na lengo la uwajibikaji.
Alieleza kuwa hoja nyingi za kuwang’oa viongozi zinatokana na vita vya kisiasa katika kaunti, na si makosa yanayostahili kutumiwa kumwondoa mtu madarakani.
“Hoja nyingi hizi zinahusiana na siasa chafu katika kaunti zetu; kuna migogoro ya makundi, masuala ya urithi wa uongozi na si kila mara huwa ni kwa sababu ya usimamizi mbaya,” alisema Gavana wa Wajir.
Alisisitiza kuwa kuna ukosefu wa uwazi kuhusu mfumo wa kisheria wa mchakato wa kuondoa viongozi, akibainisha kuwa mpaka kati ya sababu za kisheria na kisiasa za kuondoa kiongozi bado haueleweki.
Akikosoa matumizi ya hoja za kuondoa viongozi kama silaha ya kulipiza visasi vya kisiasa, Abdullahi alisema hatua hiyo inapaswa kuwa ya mwisho kabisa baada ya njia nyingine kushindikana.
“Kuondoa kiongozi madarakani kunapaswa kuwa hatua ya mwisho.
“Hatuwezi kutumia mchakato huo kama silaha ya kwanza katika vita vya kisiasa. Hata tafsiri ya nini ni ‘matumizi mabaya ya ofisi’, ‘ukiukaji mkubwa wa sheria’, au ‘ukiukaji wa Katiba’ haieleweki vizuri. Hata mawakili hawajakubaliana iwapo ni mchakato wa kisheria au wa kisiasa,” alisema.
Seneta wa Kakamega, Boni Khalwale, alisema kuwa kushindwa kwa hoja nyingi kutokana na masuala ya kitaratibu kunaonyesha haja ya kuandaliwa kwa mwongozo rasmi kuhusu jinsi ya kuendesha mchakato huo katika mabunge ya kaunti.
Alisema madiwani wamekuwa wakizingatia sababu za kuondoa gavana huku wakisahau kufuata utaratibu sahihi wa mchakato huo.
“Hoja nyingi zilizoshindwa zimeanguka kwa sababu ya taratibu. Hivyo basi kuna haja ya dharura ya kuwa na mwongozo wa kuwasaidia madiwani. Hatuwezi kuwalaumu magavana wakati mchakato mzima wa kuwaondoa si halali,” alisema Khalwale.
Kiranja huyo wa Wengi katika Seneti pia alieleza kuwa madiwani wamekuwa wakishindwa kutoa ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa wamefikia kiwango cha thuluthi mbili kinachohitajika katika hoja ya kumuondoa kiongozi.
“Kesi ya Gavana Mutai ni mfano mzuri; walishindwa kuonyesha ushahidi kwamba thuluthi mbili ya madiwani walipiga kura ya kumuondoa. Japokuwa madai ya matumizi mabaya ya ofisi na ufujaji wa pesa yalikuwepo, utaratibu ndio uliwanyima ushindi,” aliongeza.