Habari za Kitaifa

Kaunti ya Nairobi kulipa wakili nusu bilioni baada ya kushindwa kesi

Na  JOSEPH WANGUI September 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Serikali ya Kaunti ya Nairobi itamlipa wakili mmoja shilingi nusu bilioni baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali kesi iliyolenga kuzuia malipo ya huduma. Wakili huyo alidai Sh498.7 milioni kwa huduma za kisheria alizotoa miaka 18 iliyopita.

Bw Samson Masaba, anayefanya kazi chini ya jina la kampuni ya Munikah & Co Advocates, alipata ushindi baada ya Mahakama Kuu kukataa ombi la kaunti la kutaka malipo hayo ya huduma zilizotolewa 2006 yafutiliwe mbali.

Wakati huo, jiji lilikuwa likisimamiwa na Baraza la Jiji la Nairobi.

“Mlalamishi ameshindwa kuonyesha kosa lolote la kimsingi ambalo lingefanya mahakama hii iingilie kati. Madai kuwa mshtakiwa anatafuta kulipwa mara mbili kwa kazi ile ile si ya kweli na hayajaungwa mkono na rekodi yoyote,” alisema Jaji Helene Namisi.

Kiini cha mzozo huo ni kuwa wakili huyo alipewa Sh60.7 milioni kama malipo kwa kuiwakilisha Baraza la Jiji kwenye kesi iliyohusiana na kodi za ardhi.

Kwa mujibu wa serikali ya kaunti, wakili huyo hakustahili kudai Sh498.7 milioni zaidi kwa kazi ya kisheria iliyofuatia baada ya kesi hiyo kuendelea.

Uamuzi wa mahakama unajiri wakati ambapo serikali ya Kaunti ya Nairobi inakabiliwa na mzozo mwingine na wakili Donald Kipkorir kuhusu malipo ya Sh1.3 bilioni kwa huduma za kisheria alizotoa kwa lililokuwa Baraza la Jiji mwaka wa 2012 katika kesi ya umiliki wa ardhi.

Mzozo huo unafanana na kesi nyingine ya mwaka 2017 ambapo kaunti hiyo iliagizwa kumlipa Profesa Tom Ojienda Sh264 milioni kwa kuiwakilisha katika kesi tano mwaka 2014.

Katika kesi ya Bw Masaba, kiasi hicho cha fedha kimekuwa kikijadiliwa mahakamani hapo awali, huku uamuzi mmoja wa Juni 2022 ukionyesha kuwa kiasi hicho kilikuwa kimepanda hadi Sh800 milioni.

Stakabadhi za mahakama zinaonyesha kuwa wakili huyo aliajiriwa na Baraza la Jiji la Nairobi mwaka wa 2003 kufungua kesi kwa niaba yake ya kudai kodi kutoka kwa Kamishna wa Ardhi. Kwa kazi hiyo, alilipwa Sh60.7 milioni mnamo Januari 2007.

Hata hivyo, aliteuliwa tena Julai 2007 baada ya Mwanasheria Mkuu kuishtaki Baraza la Jiji akidai Sh13 bilioni. Dai hilo la lilikuwa majibu kwa kesi ya awali ya 2003 na Baraza likampa wakili huyo maagizo mapya ya kuitetea.

Wakili huyo aliwakilisha mteja wake kwa mafanikio kwa gharama ambayo ilikadiriwa kuwa Sh498.7 milioni mnamo Agosti 2012.

Pesa hizo hazikulipwa na mnamo Februari 16, 2024, kaunti iliwasilisha kesi katika Mahakama Kuu kutaka uamuzi wa malipo hayo ubatilishwe, ikidai kuwa ni kosa kumlipa wakili huyo mara mbili.

Walidai kuwa madai ya Mwanasheria Mkuu hayakuwa kesi tofauti inayostahili gharama mpya. Hoja nyingine ilikuwa kuwa kudai malipo mara ya pili kulikuwa kinyume cha sheria na njama ya kumtajirisha wakili kwa pesa za umma.

Hata hivyo, wakili alijibu kwa kusema kuwa malipo hayo ya pili yalikuwa halali kwa kuwa yalitokana na maagizo tofauti ya kuitetea Baraza dhidi ya madai mapya ambayo yaliwasilishwa baada ya kesi ya awali kumalizika.

Alieleza kuwa ilikuwa sawa na kesi huru dhidi ya mshtakiwa na kwamba wakili ana haki ya kutoza ada tofauti za maagizo ya kesi na kutetea mteja tofauti.

Jaji Namisi alikubaliana naye, akieleza kuwa malipo ya kwanza yalikuwa kwa ajili ya kuendesha kesi ya awali, ilhali ya pili yalikuwa ya kuitetea Baraza dhidi ya kesi ya pili.

“Hizi zilikuwa kazi mbili tofauti zenye maagizo tofauti. Madai ya njama ya kufuja pesa za umma ni mazito na hayapaswi kutolewa kwa wepesi. Kwa ushahidi ulio mbele yangu, madai haya hayajaungwa mkono,” alisema jaji huyo.

Alibainisha kuwa kutetea dai hilo hakukuwa mwendelezo wa kazi ya awali, bali kulikuwa kazi mpya kabisa.

“Kazi ya kuchambua, kujibu na hatimaye kushinda kesi ya kiwango hicho ni tofauti, ni kazi ya kipekee na ya kiwango kikubwa. Hivyo basi, mshtakiwa alikuwa na haki ya kuwasilisha madai tofauti ya gharama kwa kazi hiyo mpya,” alisema Jaji Namisi.

Uamuzi huu unaweka msingi mpya wa kutofautisha ada za mawakili kwenye kesi jambo ambalo huenda likaathiri mizozo ya baadaye kuhusu malipo katika sekta ya umma.