Ataka Bunge izuiwe kurekebisha sheria ya uhalifu wa mtandao
Mwanamume mmoja amewasilisha ombi katika Mahakama Kuu ya Eldoret, akitaka mahakama hiyo izuie Bunge la Kitaifa kujadili na kufanyia marekebisho Sheria ya Uhalifu wa Mitandao na Matumizi Mabaya ya Kompyuta.
Kupitia kwa wakili wake Charles Nyamweya, Sammy Ekhali aliambia mahakama kuwa marekebisho yanayopendekezwa yanahatarisha uhuru wa kuabudu unaolindwa na Katiba ya Kenya.
Bw Ekhali alishtumu Bunge kwa kutumia kisingizio cha kukabiliana na itikadi kali za kidini kama njia ya kuwakandamiza Wakristo, hasa baada ya kisa cha Shakahola kilichosababisha msukumo wa mageuzi ya kidini.
‘Kuna hatari ya serikali kutumia Bunge kuwakandamiza Wakristo na kuingilia masuala ya dini kwa mtazamo wa kiimla, bila kuwashirikisha wadau wote muhimu. Marekebisho haya yanalenga kuvunja uhuru wa kuabudu,’ alisema Bw Ekhali kupitia hati ya kiapo iliyowasilishwa mahakamani.
Mlalamishi huyo anataka mchakato huo kusitishwa hadi pale ambapo ushiriki wa umma utafanyika kwa njia ya haki na wazi.
Aidha, alikanusha madai ya Bunge kuwa wadau wote walihusishwa katika mchakato huo, akisisitiza kuwa viongozi wa kidini hawakushirikishwa ipasavyo.
‘Itikadi kali za kidini haziwezi kukomeshwa kwa serikali kusimamia madhabahu ya makanisa. Suluhisho la kweli ni kuruhusu taasisi za kidini kujisimamia kwa mujibu wa maandiko matakatifu,’ aliongeza.
Bw Ekhali alidai kuwa kuna nia fiche ya serikali kupitisha sheria ambazo zitadhoofisha Wakristo na kufungua mwanya wa kuhalalisha ibada zisizokubalika, ikiwemo ibada za kishetani.
Pia alisema kuwa maoni yaliyokusanywa na jopo la kuchunguza masuala ya dini baada ya tukio la Shakahola hayajazingatiwa katika marekebisho hayo.
Mahakama Kuu ya Eldoret tayari imepokea ombi hilo na kuamuru kuwa stakabadhi husika ziwasilishwe kwa washtakiwa ambao ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bunge la Kitaifa na Seneti.
‘Ombi hili limepokelewa kama la dharura. Stakabadhi za kesi hii ziwasilishwe kwa Mwanasheria Mkuu, Bunge la Kitaifa na Seneti kabla ya tarehe ya kusikizwa kwa kesi,’ aliamuru Jaji Robert Limo.
Jaji Limo ameagiza kesi hiyo isikilizwe Septemba 10.