Makataa ya hospitali za kibinafsi nchini kufuatia nuksi ya SHA
HOSPITALI za kibinafsi kote nchini zimepatia serikali makataa ya siku 14 kulipa malimbikizi ya madeni ya huduma za afya, la sivyo zitasitisha huduma, hatua itakayolemaza mfumo wa afya nchini.
Muungano wa Hospitali za Kibinafsi Mashinani na Mijini (RUPHA) jana ulitoa ilani ya mgomo kwa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), ukisema hali ya huduma za afya iko hatarini.
Notisi hiyo inaanza rasmi Ijumaa, Septemba 5.Akizungumza na wanahabari jijini Nairobi, Mwenyekiti wa RUPHA, Dkt Brian Lishenga, alisema hospitali zimelemewa kwa kutolipwa madeni ya jumla ya Sh76 bilioni ambazo bado hazijalipwa na serikali.
“Tuko tayari kuvumilia hali hii kwa siku 14 zaidi. Baada ya hapo, tuna chaguo mbili pekee: tuporomoke na mali yetu ipigwe mnada, au tulipwe na tuendelee kuhudumia Wakenya,” alisema Dkt Lishenga.
Deni hilo linajumuisha Sh33 bilioni zinazodai Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) iliyovunjwa, na Sh43 bilioni chini ya mfumo mpya wa SHA.Muungano huo unaitaka serikali ilipe angalau nusu ya deni hilo la SHA ndani ya muda wa wiki mbili zijazo.
Katika kipindi hicho cha notisi, hospitali zitaanza kutekeleza mapendekezo ya Shirika la Huduma za Afya Nchini (KHF), ambayo yanawataka wagonjwa kusaini barua za kukubali kulipa binafsi iwapo SHA haitalipa, au kufuatilia malipo yao moja kwa moja kwa mamlaka hiyo.
Dkt Lishenga alielezea kusikitishwa na kimya cha serikali kuhusu changamoto zinazokumba SHA, akionya kuwa huduma za afya huenda zikasambaratika kabisa ndani ya miezi mitatu ijayo.
“Tayari miezi sita imepita tangu Rais William Ruto atangaze kuwa serikali italipa hospitali zinazodai chini ya Sh10 bilioni, lakini hospitali bado hazijalipwa,” alisema. “Hatutaki kusubiri hospitali zifungwe kabisa kama ilivyotokea kwa Hospitali ya St Mary’s Mumias, ndipo hatua zichukuliwe kuziokoa,” aliongeza.