Watu saba wako kwenye rada ya polisi kuhusu mauaji Kwa Binzaro
WAPELELEZI wanachunguza namna mabaki ya dhehebu la Shakahola yalivyorejea kwa siri katika eneo la Kwa Binzaro, ndani ya shamba la Chakama, ambapo wafuasi walirudia kufunga hadi kufa na kuzikwa kwa siri kwenye makaburi ya kina kifupi, hali iliyowasha tena kumbukumbu ya mauaji ya kikatili ya mwaka 2023.
Uchunguzi umebaini uhusiano mkubwa kati ya washukiwa wa vifo vipya na mauaji ya Shakahola, ambapo zaidi ya wafuasi 450 wa kanisa la Good News International (GNI) linalohusishwa na mhubiri tata Paul Mackenzie waliangamia.
Hadi sasa, wapelelezi wakiongozwa na mkurugenzi wa kitengo cha mauaji Martin Nyuguto, kwa kushirikiana na wanapatholojia wa serikali Dkt Johansen Oduor na Dkt Richard Njoroge, wamefukua miili 34 kutoka makaburi na kukusanya sehemu zaidi ya 100 za miili zilizotapakaa msituni.
Serikali ilisitisha kwa muda zoezi hilo wiki iliyopita baada ya operesheni ya wiki moja iliyoonyesha siri za kutisha za Kwa Binzaro zilizokuwa zikifichwa na vichaka vyenye miiba mikali.
Hata hivyo, uchunguzi wa msitu huo mkubwa unaendelea, huku maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) wakiendelea kuchunguza uwepo aburi mengine. Wakati operesheni ilisimamishwa, idadi ya miili ilikuwa 32, lakini kufikia Jumatano, miili miwili zaidi ilikuwa imepatikana na kufanya jumla kuwa 34.
Wapelelezi wanaamini idadi ya waliokufa inaweza kuzidi 50, huku uchunguzi wa awali ukionyesha kwamba mafundisho ya kiunabii ya Mackenzie yaliyoendelea kuenezwa hata baada ya kukamatwa kwake ndiyo yaliyowafanya waathiriwa wa Kwa Binzaro kuendelea kufuata dhehebu hilo.
Kwa sasa, watu 11 wako kizuizini na wanasaidia polisi katika uchunguzi huku serikali ikijaribu kuelewa namna dhehebu hilo liliweza kujipanga upya hata baada ya Shakahola kuwekwa chini ya ulinzi mkali.
Miongoni mwa wanaochunguzwa ni mshukiwa mkuu ambaye ni ndugu wa karibu wa mmoja wa washtakiwa wakuu katika kesi ya mauaji ya Shakahola. Wawili hao waliendelea kuwasiliana baada ya operesheni ya 2023 iliyopelekea mamia ya watu kuokolewa na viongozi kadhaa wa dhehebu hilo kukamatwa.
“Alikuwepo msituni Shakahola. Alikutana na mmoja wa viongozi wa GNI huko Kisumu wakati wa kongamano . Baadaye aliokolewa Shakahola mwaka 2023. Sijui aliwezaje kurejea tena Kwa Binzaro,” mdokezi mmoja alisema.
Wakati jamaa huyo alikamatwa na kufunguliwa mashtaka pamoja na Mackenzie, mshukiwa huyo aliweza kujinasua. Polisi wanasema haki ya wafungwa kuwasiliana na jamaa zao huenda ilitumika vibaya kuendeleza misimamo ya kigaidi.
Akizungumza mbele ya Mahakama ya Watoto ya Tononoka, Mkuu wa Gereza la Shimo la Tewa, Abdi Willy Adan, alisisitiza kuwa haki ya mawasiliano ipo, akibainisha kwamba kundi la Mackenzie lilikosa siku yao ya kupiga simu kwa sababu walikuwa mahakamani, si kwa kunyimwa haki hiyo.
Waziri wa Usalama wa Ndani, Bw Kipchumba Murkomen, alisema hivi karibuni kuwa Mackenzie ameendelea kuwasiliana na baadhi ya wafuasi wake akiwa kizuizini.Kwa mujibu wa serikali, Mackenzie alipiga simu kwa mmoja wa washukiwa waliokamatwa baadaye kuhusiana na vifo vya Kwa Binzaro na kumuombea kabla hajatiwa mbaroni.Mtu huyo alikuwa miongoni mwa mamia waliookolewa kutoka msitu wa Shakahola mwaka 2023.“Tunataka kufahamu jinsi mtu tuliyemuokoa mwaka 2023 alirejea tena Kwa Binzaro,” alisema Bw Murkomen.
Uchunguzi umebaini pia kuwa wengi wa washukiwa 11 walioko kizuizini wana uhusiano wa moja kwa moja na mauaji ya Shakahola. Uchunguzi umebaini kuwa baada ya dhehebu hiyo kusambaratishwa Shakahola, wafuasi waliohepa au kunusurika walijipanga upya na kuanza kueneza mafundisho ya Mackenzie, kisha wakahamia ndani zaidi ya msitu ili kuepuka kunaswa.
Mwanamke mmoja alisema alishangazwa kusikia kuwa mumewe, ambaye alidhani alikufa Shakahola, amekamatwa huko Kwa Binzaro.Alisema aliishi na mumewe msituni pamoja na watoto wao watano kabla ya kuamua kuondoka baada ya miezi mitatu.“Sikufurahishwa nilipoona watoto wangu wakikosa chakula. Nililazimika kufanya uamuzi mgumu wa kuondoka nao. Mume wangu alibaki msituni,” alisema.
Kwa Binzaro na Shakahola ziko ndani ya shamba kubwa la Chakama, umbali wa takriban kilomita 30 kati yao. Polisi wanaamini kwamba wakati serikali ilipozingatia kulinda Shakahola, wafuasi wa dhehebu hilo walihamia maeneo ya ndani zaidi yasiyo na shughuli nyingi za kibinadamu, na yanayojulikana zaidi kwa wanyama pori kama ndovu na fisi, hali iliyowafanya kupata maficho salama.