Itakuwa ‘faya’ si ‘faya’? Ushawishi wa Kindiki Mt Kenya Mashariki kupimwa Mbeere
NAIBU wa Rais, Prof Kithure Kindiki sasa ana kibarua kigumu cha kuhakikisha kuwa UDA inatwaa kiti cha Mbeere Kaskazini baada ya chama hicho kumtaja mwaniaji wake wikendi.
Mnamo Jumamosi, UDA ilimtangaza Leonard Muthende kuwa mwaniaji wake kwenye uchaguzi huo mdogo ambao utaandaliwa Novemba 27.
“Ningependa kuwashukuru watu wa Mbeere Kaskazini kwa kuamua kumuunga mkono mwaniaji wa UDA kuwa mbunge wenu. Wawaniaji wengine saba wamefanya vyema kuungana na kuamua kumuunga mkono Muthende kama mgombeaji wetu,” akasema Prof Kindiki katika hafla ya kumtambulisha mwaniaji huyo.
Mbali na Bw Muthende, wawaniaji wengine ni Duncan Mbui ambaye aligura DCP na sasa atawania kama mwaniaji huru na Newton Karish wa DP ambaye anaungwa mkono na viongozi wa upinzani.
Kutambulishwa kwa Bw Muthende almaarufu ‘Leo’ sasa kunafungua uwanja wa kampeni, Prof Kindiki akiwa na kibarua cha kuhakikisha mrengo wa serikali unapata ushindi.
Naibu wa Rais atategemea sana Waziri wa Utumishi wa Umma, Geoffrey Ruku, Gavana Cecily Mbarire na Mbunge wa Mbeere Kusini Nebart Muriuki kuhakikisha kuwa UDA inawahi ushindi kwenye kura hiyo.
“Ningependa kuwarai msiwasikilize watu ambao wanawaambia mpinge serikali. Hawana ajenda, manifesto yao ni fujo na lazima muwonyeshe kivumbi katika uchaguzi huu mdogo,” akaongeza Prof Kindiki.
“Wewe (Leonard) ni sawa na waliokuwa wakimezea mate kiti hiki ambao wamebadili azma yao ili kukuunga mkono. Shirikiana na viongozi wote kuhakikisha kuwa wakazi wa Mbeere Kaskazini wanapata huduma bora na kuendelea kunufaika kwa miradi ya serikali,” akamwambia Bw Muthende.
Wachanganuzi wanasema kura hii ni muhimu kwa Prof Kindiki na kundi lake kwa sababu itaonyeshahali kamili, iwapo Rais William Ruto bado anaungwa mkono kwa dhati eneo hilo au aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua amempiku katika siasa za eneo hilo.
“Baada ya mwaniaji wa UDA kutangazwa, karata iko mikononi mwa Prof Kindiki na itategemea jinsi ambavyo ataicheza. Kinyume na upinzani ambao hauna chochote cha maana, Naibu wa Rais ana miradi na vishawishi vingine vya serikali ambavyo anaweza kuvitumia kuhakikisha UDA inapata ushindi,” akasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati anayeongeza kuwa ushindi wa mwaniaji wa UDA utakuwa kigezo muhimu cha kujua iwapo serikali bado iko kifua mbele katika siasa za Mlima Kenya Mashariki.
Aidha, ushindi huo, anafafanua, utadokeza uwezekano wa Prof Kindiki kudumisha nafasi yake kama mgombeaji mwenza wa rais katika kura ya 2027.
Mbeere Kaskazini inapakana na Tharaka-Nithi ambako ni nyumbani kwa Prof Kindiki.
Baada ya kuonekana kupoteza Mlima Kenya, Rais Ruto ameonekana kama anayeegemea sana maeneo ambako mshirika wake mpya Raila Odinga alipata uungwaji mkono katika kura ya mwaka wa 2022.