Makala

Je, unaweza kupikia kwa makaa ya kinyesi cha punda?

Na KALUME KAZUNGU September 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WADAU wa utalii mara nyingi wamelalamikia kukithiri kwa uchafu unaochangiwa na kutapakaa ovyo kwa kinyesi cha punda kisiwani Lamu.

Mji wa kale wa Lamu ni kivutio kikuu cha watalii ila usafi wake umekuwa ukitiliwa shaka kutokana na idadi kubwa ya punda wanaoishi eneo hilo ambao husababisha kero kwa kudondosha kiholela kinyesi chake mitaani na vichochoroni.

Ni kutokana na changamoto hiyo ambapo kundi moja la vijana kisiwani humo limejitokeza na ubunifu wa kugeuza kinyesi cha punde na kukitumia kama makaa ya kupikia mapochopocho.

Vijana hao wa kundi la Lamu Arts and Theatre Alliance (LATA) waliibuka na ubunifu huo mwaka 2021 baada ya kupokea mafunzo kutoka kwa wakfu wa Al-Khair kutoka Uingereza.

Kundi la Lamu Arts and Theatre Alliance (LATA) likimakinikia uundaji makaa yatokanayo na kinyesi cha punda. Picha|Hisani

Mbali na mbinu hiyo kuwa mfumo wa uzalishaji kawi salama na usio na madhara yoyote kwa mazingira, pia umesaidia pakubwa kuimarisha usafi wa mji wa kale wa Lamu.

Mshirikishi wa kundi la vijana la LATA, Bw Said Hassan, anasema awali walikuwa wameanzisha kampeni ya kukusanya kinyesi cha punda na takataka zingine mitaani na majumbani, lengo kuu likiwa ni kuikomboa Lamu kutoka kwa kisunzi na kero la uchafu.

“Mapema 2021, tulizindua kampeni ya kibinafsi kama kundi kwa jina ‘Weka Lamu Safi’. Tulizurura mitaani na kwenye vishoroba vya mji wetu wa kale kukusanya na kuzoa kinyesi cha punda na taka zingine. Miezi kadhaa baadaye tukapokea mafunzo ya jinsi ya kutengeneza makaa kutoka kwa kinyesi cha punda,” akasema Bw Hassan.

Baadaye wakfu huo wa Al-Khair uliwatunuku wanachama wa LATA mtambo maalum wa kukorogea kinyesi cha punda na kuunda makaa.

Vijana wa kundi la Lamu Arts and Theatre Alliance (LATA) wakitengeneza makaa ya kupikia kupitia kinyesi cha punda. Picha|Hisani

“Tulikaa kama wanachama na kuibuka na mpango wa kutengeneza makaa tukitumia kinyesi cha punda, maji, mchanga, unga na unga wa makaa,” akasema Bw Hassan.

Fatma Mohamed, mmoja wa viongozi wa LATA, alisema mradi umenoga si haba tangu kuzinduliwa kwake katikati ya mwaka 2021.

Kulingana na Bi Mohamed, wao hutengeneza kati ya kilo 50 na 60 za makaa ya mchanganyiko wa kinyesi cha punda.

Kilo moja ya makaa hayo huuzwa kwa bei ya mtaani ya Sh80.

“Mradi umeunda ajira kwa sisi vijana. Karibu wanachama 15 wako ndani ya mradi huu. Kwa mwezi hatukosi kati ya Sh60,000 na Sh72,000 kupitia uuzaji wa hayo makaa ya kinyesi cha punda. Tunatumia hela kuendeleza ajenda za kikundi na kukimu mahitaji yetu binafsi pia,” akasema Bi Mohamed.

Bi Salwa Bakari alisema ni kutokana na mradi huo, ambapo vijana wamejishughulisha hivyo kuepuka kupotelea kwenye janga la mihadarati.

Makaa yaliyoundwa kupitia kinyesi cha punda Lamu. Mbali na kuboresha usafi wa mji, mradi huo pia umeleta ajira kwa vijana.
Picha|Hisani

Afisa wa Udhibiti wa Mazingira Kaunti ya Lamu Bw Is’haq Khatib naye alisifu ubunifu huo, akiutaja kuwa ni wenye kuimarisha usafi kwenye mji wa kale.

Bw Khatib alisema serikali ina mpango wa kuendeleza miradi zaidi sawia ambayo ni yenye kulinda mazingira, kuunda ajira kwa vijana na kuboresha usafi mjini.

“Mradi umesaidia kupiga jeki afya na usafi wa wakazi kwa jumla. Hakuna tena kinyesi cha punda kuonekana kikitapakaa vichochoroni na mitaani mjini. Siku za hivi karibuni usafi wa mji wetu umeimarika pakubwa, hivyo utalii kunoga pia. Tunapongeza mradi huo,” akasema Bw Khatib.