Habari

Gavana wa Machakos asimamisha kazi maafisa 36 kwa tuhuma za ufisadi

Na SAMMY KIMATU September 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

GAVANA wa Machakos Wavinya Ndeti amewasimamisha kazi maafisa 36 wa kaunti wanaokabiliwa na tuhuma za ukiukaji wa maadili katika ukusanyaji wa mapato.

Akizungumza katika afisi yake, Gavana Ndeti alifichua kuwa hatua hiyo imechukuliwa kufuatia ripoti za kuaminika zinazoonyesha kuwepo kwa visa vya utovu wa nidhamu, vikiwemo kuripoti mapato pungufu, utoaji wa risiti ghushi, kupotea kwa fedha za umma, na ushirikiano wa kifisadi kati ya baadhi ya maafisa na wananchi.

Maafisa waliosimamishwa kazi wanatoka katika idara mbalimbali zikiwemo Utawala, Biashara, Leseni za Pombe, Uhasibu, Mapato, Ukaguzi, Huduma za Zimamoto, na Wahasibu wa Malipo.

“Wameelekezwa kukabidhi majukumu yao mara moja kwa maafisa wakuu wa idara husika na kuacha kuhusika katika shughuli zozote kwa niaba ya serikali ya kaunti,” alisema Gavana Ndeti.

“Kesi zao zimepelekwa kwa taasisi husika — yaani Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) — kwa hatua zaidi na urejeshaji wa fedha za umma,” aliongeza.

Gavana Wavinya alisisitiza kuwa utawala wake umejikita katika vita dhidi ya ufisadi na anadhamiria kurejesha uwajibikaji katika utumishi wa umma.

“Utumishi wa umma lazima ujengwe juu ya uwazi, uwajibikaji, na uadilifu. Ni lazima tubadilishe utamaduni wa kuendeleza ufisadi na kuanza kuthamini uaminifu,” alisisitiza.

Aidha, aliwahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika vita dhidi ya ufisadi.

“Wananchi wana jukumu la kukataa kushiriki katika vitendo vya kifisadi, kuuliza maswali wanapokuwa na mashaka, na kuunga mkono juhudi hizi. Lazima tushinde vita hivi kwa pamoja,” alisema.

Kuhusu madeni yaliyosalia, gavana huyo alieleza kuwa serikali yake inashughulikia madeni yaliyorithiwa kutoka kwa utawala uliopita, ambayo yanakadiriwa kufikia Sh4.2 bilioni.

Aliahidi kuwa madai yote halali yatalipwa baada ya uthibitisho, na hatua zinaendelea kuchukuliwa kupunguza madeni yaliyopo kwa Mamlaka ya ukusanyaji Ushuru ya Kenya (KRA).