Habari za Kitaifa

Nusu ya Wakenya walidhulumiwa na polisi kati ya 2022-2024, ripoti yafichua

Na NDUBI MOTURI September 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ASILIMIA 42.9 ya Wakenya wameathiriwa moja kwa moja na ukatili au dhuluma za polisi kati ya 2022 hadi 2024, kulingana na ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la International Justice Mission (IJM).

Takwimu hizi zinabainisha hali ya kusikitisha iliyo kwenye idara ya usalama licha ya mageuzi ya kikatiba na taasisi mbalimbali za usimamizi.

Utafiti huo unaonyesha kuwa, rushwa na ulaghai ndio aina kuu za unyanyasaji, zikiathiri asilimia 55.8 ya waathiriwa, huku asilimia 54.7 wakiripoti kunyanyaswa au kusumbuliwa kiholela.

Aina nyingine za ukatili ni pamoja na kukamatwa kiholela, kushambuliwa kimwili, na hata mauaji ya kiholela.

Wanaume ndio walilengwa zaidi, wakichangia asilimia 61.4 ya visa vilivyoripotiwa, ikilinganishwa na asilimia 38.5 ya wanawake.

Wakazi wa mijini walilengwa pakubwa zaidi—asilimia 75.9 ya waathiriwa walitoka mijini, huku maeneo ya mashambani yakichangia asilimia 24.1 pekee.

Mkurugenzi wa IJM nchini Kenya, Bw Vincent Chahale, aliitaka Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) kuboresha mafunzo kuhusu heshima kwa haki za kibinadamu.

“Waathiriwa wa ukatili wa polisi wanastahili haki. Ripoti hii inasisitiza umuhimu wa kuboresha huduma ya polisi, na haya yote huanzia katika mchakato wa uajiri, unaotarajiwa kuanza siku chache zijazo,” alisema Bw Chahale.

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa Kisumu ndio eneo lililoathirika zaidi, likifuatiwa na Nairobi na Mombasa.

Vijana wenye umri wa miaka 25 hadi 34 ndio walilengwa zaidi, huku wale walio na elimu ya juu wakikumbwa zaidi na dhuluma ikilinganishwa na walio na elimu ya chini.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa, asilimia 33.1 ya waathiriwa walidhulumiwa katika maeneo ya umma nje ya makazi yao.