NPSC yaonya Wakenya kuhusu taarifa feki za usajili wa makurutu
HUKU Tume ya Kitaifa ya Huduma za Polisi (NPSC) ikijiandaa kutoa tangazo kuhusu usajili wa makurutu wapya wa polisi Alhamisi, Septemba 11, 2025, imeonya umma dhidi ya habari za kupotosha kuhusu suala hilo.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumanne jioni, mwenyetiki wa tume hiyo Amani Yuda Komora amewataka Wakenya kupuuza tangazo feki linalosambazwa mitandaoni lenye maelezo ya kupotosha kuhusu zoezi hilo.
“Tume ya Kitaifa ya Huduma za Polisi imebaini, kuwa taarifa feki kuhusu usajili inasambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikidai kutangaza usajili wa makonstebo wa polisi na kuelekeza wahusika kwa wavuti fulani haramu,” akasema.
Bw Komora alifafanua kuwa NPSC haijatoa maelezo yoyote kuhusu usajili huo akisisitiza kuwa taarifa rasmi kuhusu usajili wa makurutu wapya wa polisi itatolewa kupitia majukwaa rasmi.
“Kwa hivyo, tume ingependa kushauri umma kupuuzilia mbali habari hiyo ya kupotosha na kufafanua kuwa maelezo kuhusu usajili huo yatatolewa kupitia tovuti ya NPSC, vyombo vikuu vya habari na majukuwaa ya mitandao ya kijamii yaliyoidhinishwa,” Dkt Komora akaongeza.
Awali, mwenyekiti huyo wa NPSC na Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja waliwaambia wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Usalama kwamba maelezo rasmi kuhusu zoezi hilo yatachapishwa magazetini Alhamisi Septemba 11.
Hata hivyo, wawili hao waliwaarifu wabunge hao kwamba wanachama wa NPSC na Shirika la Kitaifa la Huduma za Polisi (NPS) watakutana “haraka iwezekanavyo” kukubaliana kuhusu tarehe ya kuendeshwa kwa zoezi hilo.
Jumla ya makurutu 10,000 wa polisi wa cheo cha konstebo wanatarajiwa kusajiliwa katika zoezi hilo kujaza nafasi zilizoachwa wazi na maafisa wanaokufa, kufutwa kazi, kujizulu na kustaafu.
“Jinsi mwenyekiti wa tume amekwisha kusema, katika mkutano tutakaofanya tutakubaliana kuhusu tarehe, mwongozo na taratibu za kufuata,” Bw Kanja akawaambia wabunge wanachama wa kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Narok Magharibi Gabriel Tongoyo.
Zoezi la usajili wa makurutu wa polisi huvutia maelfu ya wanaotaka kujaza nafasi zilizopo, kutoka pembe zote za nchini, na hivyo kushuhudia ushindani mkubwa.
Katika hali kama hiyo, visa vya utovu wa maadili huchipuza ambapo baadhi ya wanaotaka kusajiliwa huitishwa hongo ya kima cha hadi Sh300,000.
Hii ndio maana NPSC ilitunga kanuni mpya ya usajili na kupendekeza kuwa zoezi hilo liendeshwe kwa njia ya mtandao, pendekezo ambalo limepingwa na Bw Kanja pamoja na wakuu wengine wa NPS.