Jamvi La Siasa

Madiwani walivyomponda Raila mazishi ya Lempurkel

September 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MASHAMBULIZI ya moja kwa moja dhidi ya kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Bw Raila Odinga, yaliibua mzozo mkali wakati wa mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Laikipia Kaskazini, Mathew Lempurkel, ishara ya migawanyiko inayozidi kukithiri ndani ya uongozi wa chama hicho.

Diwani wa wadi ya Mukogodo Magharibi, Bw Nicholas Lempaira, aliwashangaza waombolezaji alipopanda jukwaani na kumkemea kiongozi wake wa chama kwa maneno makali, akionyesha wazi kutoridhishwa na uongozi wa ODM.

“Umetuangusha mara mbili pamoja na Mathew baada ya kutuahidi nafasi katika Bunge la Afrika Mashariki. Mathew alifungwa jela na kuteswa na polisi kwa sababu ya uaminifu wake kwa ODM. Umetuangusha Mzee, na unapaswa kutuonyesha mwelekeo ukiwa bado hai,” Bw Lempaira alisema, akivutia kelele za furaha na za kejeli kutoka kwa hadhira.

‘Tuko matatani’

Aliendelea kusema: “Kwa sasa tuko matatani. Hatujui kama tuko ndani ya UDA au katika serikali ya nusu mkate. Lakini nataka kumpongeza Edwin Sifuna kwa msimamo wake. Tunakuunga mkono na tukiona viongozi wa chama wakikugusa, sisi wa mashinani tutaondoka wote ODM.”

Bw Sifuna, ambaye ni Katibu Mkuu wa ODM, amekuwa akipinga vikali ushirikiano wa ODM na serikali ya Kenya Kwanza – mpango uliowawezesha wandani wa Bw Odinga kupata nyadhifa serikalini.

Seneta huyo wa Nairobi ameungana na viongozi vijana kama Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino, na Mbunge wa Githunguri, Gathoni Wamuchomba, chini ya vuguvugu la kisiasa la Kenya Moja, linalodai kuwa litakomboa nchi kutoka dhuluma za serikali na kuhakikisha utoaji bora wa huduma kwa wananchi.

Ingawa Bw Sifuna aliandamana na Bw Odinga kwenye mazishi yaliyofanyika katika kijiji cha Il Polei, aliepuka kuzungumzia mvutano ndani ya ODM na badala yake alitumia fursa hiyo kuitaka serikali kulipa madeni ya huduma za Bima ya Afya kwa hospitali zinazomilikiwa na Kanisa Katoliki.

Uongozi wa ODM Kaunti ya Laikipia ulijitokeza haraka kujitenga na matamshi ya diwani huyo anayehudumu kwa muhula wa kwanza, ukiyataja kuwa “ovyo, yasiyo ya heshima kwa mzee na kiongozi wa kitaifa.”

“Kama tawi la ODM, tunalaani vikali matamshi ya Lempaira dhidi ya kiongozi wetu wa chama. Kauli hizo zinaonyesha wazi kuwa Lempaira ni msaliti ambaye ni ‘fuko’ wa chama cha DCP ndani ya ODM,” alisema mwenyekiti wa ODM tawi la Laikipia, Bw John Orengo.

Bw Orengo alidai kuwa diwani huyo amekuwa akiwasiliana kwa karibu na viongozi wa chama cha Democratic Citizens Party (DCP) na hata kutembelea nyumbani kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kule Wamunyoro n ahata kuchapisha picha ya ziara hiyo kwenye mitandao ya kijamii.

“Tunao madiwani wawili wa ODM waliochaguliwa Laikipia, lakini kwa bahati mbaya hawaungi mkono ODM, na wamekuwa wakishirikiana kisiri na vyama pinzani. Kama wanajiona maarufu, tunawashauri wajiuzulu na watafute kura upya kwa tiketi ya chama kingine,” aliongeza Bw Orengo.

Ashutumu Odinga

Diwani mwenzake, Bw Sammy Lekopien (wa wadi ya Sossian), pia alimshutumu Bw Odinga kwa kumtelekeza Bw Lempurkel wakati alihitaji msaada zaidi, akitaja hilo kuwa aibu kubwa.

“Sisi wawili tu ndio madiwani wa ODM katika Bunge la Kaunti ya Laikipia. Kwa kifo cha Lempurkel, tumebaki kama mayatima. Inasikitisha kuona kuwa wanachama waaminifu hawathaminiwi baada ya kushindwa kwenye uchaguzi mkuu, jambo ambalo linakatisha tamaa wagombeaji kutumia tiketi ya ODM,” alisema Bw Lekopien.

Bw Lempurkel alitambuliwa kwa kuimarisha ODM katika eneo la Laikipia aliposhinda kiti cha ubunge mnamo 2013 kwa tiketi ya chama hicho, licha ya kuwa wakati huo chama cha TNA kilikuwa kinatawala eneo hilo.

Alishindwa mwaka wa 2017 na Bi Sarah Korere.

Hata hivyo, aliendelea kuwa mwaminifu kwa ODM hata alipokumbwa na mashtaka ya mara kwa mara kutoka kwa serikali kwa kujitokeza kutetea haki za ardhi za jamii ya Maa, hatua ambayo maafisa wa usalama walitafsiri kama kuchochea ghasia.

Wakati mmoja, alishtakiwa kwa kuwachochea wafuasi wake kuvamia mashamba ya kibinafsi.

Mbunge huyo wa zamani alifariki mnamo Agosti 24 baada ya kugongwa na gari lililotoroka, katika eneo la Ongata Rongai, Kaunti ya Kajiado.

Kabla ya kifo chake, alikuwa tayari amejiunga na chama cha DCP na alikuwa na nia ya kuwania ubunge mwaka wa 2027 kupitia chama hicho.

Ingawa marehemu alikuwa amejiunga rasmi na chama cha DCP, hakuna kiongozi wa chama hicho aliyehudhuria mazishi yake, licha ya fununu kuwa Naibu Rais Gachagua angekuwepo.

Wabunge wanne wa Laikipia walikosa kuhudhuria, wakiwemo mbunge wa eneo hilo, Bi Sarah Korere. Gavana, maseneta na wabunge kutoka Kajiado, Samburu na Narok ndio waliongoza hafla ya mazishi.