Madiwani wa Kisii waliosusia mkutano wa Ruto Ikulu watoa sababu
ZAIDI ya madiwani (MCAs) 20 kutoka Kaunti ya Kisii, wametoa sababu ya kususia mkutano na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi.
Rais Ruto alikuwa ametuma mwaliko kwa MCAs kutoka kaunti za Kisii na Nyamira, akiwataka wamtembelee ikuluni siku ya Alhamisi Septemba 11, 2025.
Wakiongozwa na Gavana wa Kisii Simba Arati, sehemu ya madiwani hao walikutana na Rais Ruto lakini baadhi yao, akiwemo Gavana wa Nyamira Amos Nyaribo walisalia nyumbani.
Wakizungumza mjini Kisii wakati mkutano wa ikulu ulikuwa ukiendelea, MCAs hao walisema safari hiyo iliyoongozwa na Gavana Arati haikuwa na umuhimu wowote wa kimaendeleo bali ni njama ya kumkata mbawa aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i.
Waziri huyo wa zamani ametangaza nia yake ya kuwania urais katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu wa 2027.
Madiwani hao walidokeza kwamba kwa kuwa Dkt Matiang’i ndiye mwaniaji wao wa urais katika uchaguzi wa 2027, hawangethubutu kukanyaga ikuluni kwani kufanya hivyo ni sawia na kuisaliti jamii ambayo imempendekeza awanie wadhfa huo.
Madiwani Wilfred Monyenye (Kisii ya Kati) na Dennis Ombachi (Marani), walimsuta Arati na kusema hakuna lolote atakaloleta kutoka kwa mkutano huo.
Bw Monyenye aliuliza ni kwa nini Rais Ruto anazidi kualika watu kutoka kaunti za Kisii na Nyamira mara kwa mara.
“Ni hivi majuzi, zaidi ya watu 6,000 kutoka eneo letu walipelekwa na wajumbe wake wa huku eti wanaenda kukwamua maendeleo. Ikiwa lengo la mkutano huo lilikuwa kweli kukwamua maendeleo, mbona tena mkutano mwingine?” Bw Monyenye aliuliza.
Diwani huyo alitumia fursa hiyo kumweleza Dkt Ruto kutowazia kura za Gusii tena na kusema kuwa kura hizo tayari zimemwendea Dkt Matiang’i.
Kauli ya Bw Monyenye iliungwa mkono na diwani maalum Bathseba Sanaya aliyesema Dkt Matiang’i ndiye chaguo bora la urais kwa kuwa amekubalika na jamii zingine. Bi Sanaya aliisihi jamii ya Abagusii kumuunga mkono Dkt Matiang’i mia fil mia.
James Ondari Paradiso, diwani wa Boochi Tendere alisema ni dhahiri Bw Ruto alikuwa amefeli kuwatumikia Wakenya na hivyo basi watatafuta chaguo lingine mwaka 2027.
Madiwani Walter Mochache (Kiogoro) na Caren Magara (maalum) walisema watu kutoka Gusii wamekutana na Rais mara nyingi lakini hawatimizii ahadi ambazo anawatolea.
“Tumekutana na rais katika ikulu ndogo za Kisii na Kakamega. Tulikaa na yeye na tukamweleza kuhusu maendeleo hayo ambayo wenzetu wamesema wameenda kuyakwamua lakini hajayatekeleza. Ndugu zetu kutoka Luo Nyanza, wao wanafanyiwa kila kitu lakini sisi tunaambiwa twende kuyachukua kwa nini?” Bw Mochache aliuliza.
Diwani Lilian Gor alimkashifu Bw Arati na kusema ni kinaya kuwa gavana huyo aliongoza ujumbe uliokwenda kukwamua maendeleo ilhali mkuu huyo wa kaunti hatumii pesa za mgao wa kaunti kufanikisha miradi mbali mbali.
“Ninataka kumwambia gavana kuwa akishamaliza kutafuta maendeleo hayo ikulu, akija hapa awalipe wanakandarasi waliotoa huduma kwa serikali ya Kisii. Pesa zinazidi kulala katika akaunti, watu wanakufa njaa na mwishowe pesa hizo zinarudi Nairobi,” Bi Gor alisema.
Diwani wa Masimba Bouse Mairura aliwataka wenzake waliomtembelea rais ikuluni kuonyesha umma maendeleo waliyopewa pindi tu watakapowasili katika maeneo wakilishi.
“Ikiwa ni pesa walipewa, waambieni pia wawagawie pesa hizo mle kwa kuwa uchumi wetu ni mgumu. Na ikiwa ni maendeleo, waambie wawaeleze yaliko,” Bw Mairura alisema.