Safaricom Chapa Dimba All Stars yaendelea kufinya klabu za Uhispania
TIMU ya Safaricom Chapa Dimba All Stars iliendeleza ushindi katika mechi zake za pili za kirafiki dhidi ya klabu za Uhispania, uwanjani Federación Aragonesa de Futbol na Zaragoza Playing Grounds mnamo Alhamisi.
Katika soka ya wavulana, Chapa Dimba ililemea SD Valdefierro 6-0 kupitia mabao ya Brian Aroko na Armstrong Omondi waliofunga mawili kila mmoja huku Lokonde Mwale na Felix Manguti wakitinga moja moja.
“Huwa nachukulia kila mechi kama ya lazima kushinda. Vijana wako tayari kufanya kazi, wamekuja hapa kuonyesha vipaji vyao ndiyo maana wanacheza vizuri sana. Kushinda si kitu cha uhakika, lakini ukiwa na mpira mzuri unajiongezea nafasi. Ndio maana tumekuwa tukivuna ushindi mnono katika michuano yetu,” alitanguliza Evan Oketch, kocha wa wavulana wa All Stars.
Akaongeza: “Mchezo wa leo (Alhamisi) ulikuwa mzuri sana. Vijana walianza kwa nguvu na kudumisha kasi hadi mwisho. Katika mechi ya kwanza tuliruhusu bao, lakini leo tulihakikisha hatujafungwa lolote.”

Kwa upande wa wasichana, Chapa Dimba All-Stars Girls waliibuka na ushindi wa 6-4 dhidi ya wenyeji Zaragoza CFF kupitia mabao ya Swaumu Masungo (matatu), Hellen Mito (mawili) na Sharon Asado.
“Mchezo wa leo ulikuwa bora zaidi ikilinganishwa na ule wa kwanza uliokamilika katika sare. Tumeonyesha maendeleo makubwa na ilikuwa vizuri sana kucheza dhidi ya timu ya Uhispania. Hii ni mara yangu ya kwanza kucheza na kushinda nchini Uhispania – ndoto yangu imetimia! akasema mchezaji Sheilla Juma.
“Tumetekeleza tuliyofundishwa katika siku tatu zilizopita, kama vile kuunda nafasi na kutoa pasi kwa haraka. Ndiyo maana tuliweza kuwalemea wapinzani wetu,” alieleza.
Mechi hizo za kirafiki zilikuwa sehemu ya siku ya tatu ya kambi ya mafunzo ya kipekee ya Safaricom Chapa Dimba All-Stars yanayoendelea nchini Uhispania.
Mapema Alhamisi wachezaji walitembelea Podoactiva; makao makuu na kituo kikubwa zaidi cha tiba ya miguu na msongeo wa kimitambo wa maungo ya mwili – biomechanics kwa Kimombo – barani Ulaya, kinachopatikana Walqa Technology Park mjini Huesca.
Kituo hicho kimejikita katika utambuzi na matibabu ya matatizo ya miguu na kutembea kwa kutumia teknolojia ya kisasa, kikitoa huduma kama uchunguzi wa jinsi viungo mwilini vinasonga, soli maalum ya ndani, tiba ya miguu, upasuaji wa miguu kwa watu binafsi pamoja na huduma kwa timu za michezo ya kitaaluma.

Ziara hiyo iliwafahamisha wachezaji kuhusu njia mbalimbali za kujijengea maisha katika michezo, nje ya soka.
Kama ilivyokuwa kwa Hellen Mito na Martha Nafula – ambao waliteuliwa kujiunga na mazoezi ya timu ya watu wazima ya wanawake ya SD Huesca mnamo Jumanne – wachezaji Derrick Oketch na Aroko pia wameteuliwa kushiriki mazoezi na timu ya watu wazima ya wanaume ya SD Huesca hapo Ijumaa.
Wawili hao wataanzia katika chumba cha mazoezi wakiwa pamoja na kikosi cha watu wazima kabla kujumuika nao uwanjani kwa mazoezi ya kiufundi asubuhi.
Baadaye Ijumaa jioni timu ya wavulana itakabiliana na SD Huesca C katika mechi nyingine ya kirafiki kwenye viwanja vya akademia ya Huesca.