Ruto alivyoweka historia kukwea mlima kabla ya kuteleza
Rais William Ruto aliweka historia ya kisiasa katika eneo la Kati mwa Kenya mwaka wa 2022 kwa kuwa mgombea wa kwanza wa urais kutoka nje ya jamii ya Agikuyu aliyepata uungwaji mkono wa pamoja kutoka kwa wapiga kura wa eneo hilo.
Alipoapishwa rasmi kuwa Rais mnamo Septemba 13, 2022, eneo hilo lilijawa na matumaini kwamba safari yao ya kisiasa kuelekea “Canaani” ilikuwa imefika hatimaye, huku Dkt Ruto akichukuliwa kama mkombozi wa uongozi.
Aliwashangaza wengi kwa kupata asilimia 87 ya kura. Chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) kilinyakua karibu kila kiti kilichokuwa kinagombewa katika eneo hilo.
Kilichofanya hali hiyo kuwa ya kushangaza zaidi ni kwamba alifanikiwa kuangusha ngome ya kisiasa ya wakati huo, Bw Uhuru Kenyatta, ambaye alikuwa akimpigia debe kiongozi wa upinzani Raila Odinga kama mgombea urais, na mgombea mwenza wake akiwa Martha Karua, binti wa eneo hilo.
“Tangu uhuru, wapiga kura wetu daima wamekuwa wakipinga wagombeaji wa urais kutoka nje ya eneo hili hadi pale Dkt Ruto alipojitokeza mwaka 2022. Hili ni jambo linalofaa kufanyiwa utafiti na kurekodiwa kwa ajili ya vizazi vijavyo kuelewa jinsi lilivyowezekana,” anasema Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Kikuyu, Wachira Kiago.
Bw Kiago anasema maelezo yanayotolewa na baadhi ya wanasiasa ni kubahatisha tu, “kwa sababu wengine wengi wanaamini kwamba haikuwa siasa bali ilikuwa zaidi ni jambo la kiroho.”
“Baada ya kupitia kipindi kigumu cha machafuko ya baada ya uchaguzi wa 2007/8, hasa katika Bonde la Ufa, sisi kama jamii tulihitaji amani. Tuna hisa kubwa katika taifa hili,” anasema Bw Kiago.
Anasema kwamba Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ambayo iliwatuhumu Bw Kenyatta na Bw Ruto miongoni mwa washukiwa sita wa ghasia hizo, kabla ya kuwaachilia baadaye, “ilikuwa kama gundi iliyotufanya tutafute ushirikiano kama jamii mbili kuu zilizokuwa mahasimu wakati wa ghasia”
Anadokeza kuwa Rais wa wakati huo Mwai Kibaki, pamoja na wadau mbalimbali, walikuja pamoja kuhakikisha kuwa Bw Kenyatta na Dkt Ruto walishirikiana katika uchaguzi mkuu wa 2013 ambapo walishinda na kuingia mamlakani.
Mkuu wa zamani wa mkoa, Joseph Kaguthi, anasema, “Hatukuwa na chaguo ila kumvuta Dkt Ruto upande wetu ili tupate mafanikio mawili kwa wakati mmoja: kutuliza Bonde la Ufa ambako watu wetu wanaishi na pia kupata amani kwao na kushirikiana kutafuta mamlaka.”
Na hilo lilitimia. Bw Kenyatta akawa mgombea wa urais na Dkt Ruto mgombea mwenza. Walishinda uchaguzi huo licha ya changamoto na baadaye wakaachiliwa na ICC.
Ushirikiano kati ya Bw Kenyatta na Dkt Ruto ulikuwa wa karibu sana kiasi kwamba, labda kwa sababu ya furaha na matumaini, Rais Kenyatta aliahidi mapema kwamba angetawala kwa miaka 10 kisha amkabidhi Dkt Ruto kwa kauli maarufu ya “Kumi yangu, kumi ya William.”
Ahadi hiyo ilichukuliwa kama mtego kwa jamii ya Agikuyu. Wachanganuzi walitaka kuona ikiwa eneo hilo lingeweza kutimiza ahadi ya kisiasa, hasa kwa “mgeni”.
“Bila shaka, sisi kama jamii tunathamini uaminifu, na tunalipa mema kwa mema daima. Dkt Ruto alitusaidia kuangusha ICC na pia kumshinda Raila Odinga mwaka 2013 ili kuendelea kushikilia mamlaka. Bw Kenyatta alimhakikishia angerudisha mkono, na tukajikuta tukiwa tumenaswa na uaminifu wetu wenyewe,” anasema mlezi wa kitaifa wa Kiama kia Ma, Kung’u Muigai.
“Ingawa tulikuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu kumpigia kura Dkt Ruto mwaka 2022 kwa sababu kiongozi wake, Kenyatta, alikuwa ameonyesha kuenda kinyume na ahadi yake, heshima yetu kwa uaminifu na ahadi ilishinda, tukamkubali mwana kutoka Kamagut kama mshirika wetu wa kisiasa,” anaongeza Bw Muigai.
Dkt Ruto aliendelea hadi kumdhalilisha Bw Kenyatta, huku Bw Odinga akipata asilimia 12 pekee ya kura kutoka eneo hilo. Dkt Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua wakawa watawala wapya wa kisiasa nchini, na Mlima Kenya ukajawa na matumaini.
Mchanganuzi wa kisiasa na msomi Profesa Peter Kagwanja anasema kulikuwa na nderemo kubwa.
“Upendo wetu wa kipekee kwa Dkt Ruto ulifika kiwango kingine kabisa. Lakini kisiasa, tafsiri ni kwamba mapenzi ya watu wa Mlima Kenya kwa Dkt Ruto yalikuwa makubwa sana kiasi cha kuwafanya wawe tayari kumtupa Kenyatta wao chini kwa nia ya kuonyesha uungwaji mkono kwa serikali ya Ruto,” anasema Prof Kagwanja.
“Mapenzi haya ya upofu hayakusaidiwa na ukweli kwamba mtu tuliye mtuma kuwa naibu wa Dkt Ruto kwa jina la Gachagua hakuonyesha busara yoyote ya kudai mashauriano ya kimuundo kwanza,” anaongeza.