Dimba

Riadha za Dunia: Kenya teketeke 4x400m kabla kubanduliwa kwa kukanyaga laini visivyo

Na GEOFFREY ANENE September 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SHEREHE za Kenya baada ya kufuzu kwa fainali ya mbio mseto za kupokezana vijiti za mita 4×400 hazikudumu baada ya timu kubanduliwa kwa kosa la kukanyaga laini ya mpinzani, katika siku ya kwanza ya Riadha za Dunia 2025 mjini Tokyo, Japan, Jumamosi.

Kikosi hicho kinachoongozwa na Mary Moraa na kujumuisha Brian Tinega, Mercy Oketch na Allan Kipyego kilikuwa kimenyakua tiketi ya moja kwa moja baada ya kumaliza nambari mbili kwenye mchujo wa pili uwanja wa kitaifa wa Japan.

Kiliweka rekodi mpya ya Afrika ya dakika 3:10.73 na kufuta ile ya awali ya Afrika Kusini (3:11.16) iliyowekwa dakika chache tu katika mchujo wa kwanza.

Kenya ilianza vyema ikitokea laini ya tano kupitia Tinega ambaye alikabidhi kijiti kwa Oketch, naye akampa Kipyego aliyeziba pengo vizuri na kumpokeza Moraa.

Bingwa wa dunia katika 800m, Moraa, hakuwavunja moyo mashabiki akiongoza Kenya kumaliza ya pili nyuma ya Ubelgiji iliyomaliza kidedea kwa dakika 3:10.37.

Hata hivyo, sherehe za mashabiki na watimkaji wa Kenya zilikatizwa ghafla baada ya kutangaziwa uamuzi wa kutolewa wakati wakifanya mahojiano ya baada ya mbio.

Wakenya walipatikana na kosa la kukiuka kifungu cha TR17.23 cha Kanuni ya Riadha za Dunia, kinachotoa adhabu ya moja kwa moja ya kuondolewa mashindanoni kwa kukanyaga nje ya mstari au kukiuka laini mara kadhaa.

Tinega alihesabiwa kufanya kosa hilo mara kadhaa kwenye kona, jambo lililosababisha Kenya kutolewa moja kwa moja. Hiyo ilipisha wenyeji Japan kushiriki fainali itakayofanyika Jumamosi jioni.

Aidha, inamaanisha rekodi ya bara Afrika ya dakika 3:11.16 iliyowekwa na Afrika Kusini bado inabaki. Kenya inaweza kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.