Historia! Chebet Mkenya wa kwanza kushinda 10,000m katika Riadha za Dunia tangu 2015
KENYA imepata medali yake ya kwanza na pia ya kihistoria baada ya mshikilizi wa rekodi ya dunia Beatrice Chebet kutawala mbio za mita 10,000 kwenye makala ya 20 ya Riadha za Dunia mjini Tokyo, Japan, Jumamosi.
Chebet pamoja Janeth Chepngetich na Agnes Ngetich walikuwa wawakilishi wa Kenya katika mbio hizo za kuzunguka uwanja mara 25.
Bingwa wa Olimpiki 5,000m na 10,000m, Chebet aliibuka mshindi wa 10,000m kwa dakika 30:37.61.

Alihitaji kujituma zaidi ya kawaida katika mzunguko wa mwisho kumlemea Mwitaliano Nadia Battocletti pembamba (30:38.23) huku Muethiopia Gudaf Tsegay akaridhika na shaba (30:39.65).
Ngetich, anayeshikilia rekodi ya dunia ya kilomita 10 barabarani, alimaliza katika nafasi ya nne kwa 30:42.66 kutoka orodha ya washiriki 27. Chepngetich hakukamilisha mbio.
Supastaa!
Chebet sasa ni mwanamke wa kwanza kutoka Kenya kushinda taji la dunia la 10,000m baada ya Vivian Cheruiyot mwaka 2015 mjini Beijing, Uchina.
Waethiopia walifagia medali zote za 10,000m za wanawake katika makala yaliyopita mjini Budapest, Hungary, huku Irine Kimais akiwa Mkenya wa kwanza katika nafasi ya nne.
Medali ya 10,000m ni pekee kubwa iliyokuwa ikikosa kwenye kabati la Chebet kwani anajivunia kushinda dhahabu ya 5,000m kwenye Riadha za Afrika na Michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka 2022, Riadha za Dunia za Chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 (2018), Mbio za Nyika za Dunia (2019, 2023 na 2024), Kilomita tano kwenye Riadha za Dunia za Barabarani (2023) na 5,000m kwenye Diamond League (2024) na Olimpiki (2024).