Habari za Kitaifa

NCCK yahimiza Gen Z kujisajili kupiga kura na kuwania nyadhifa 2027

Na MAUREEN ONGALA September 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Baraza Kuu la Makanisa Nchini Kenya (NCCK) imewataka vijana wa kizazi cha Gen Z kujisajili kama wapiga kura ili kuleta mabadiliko ya uongozi wanayotamani katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Makamu Mwenyekiti wa NCCK, Josephat Kalume, amesema kuwa sauti ya vijana haitahesabiwa ikiwa hawatakuwa katika sajili ya wapiga kura. Akizungumza katika mkutano wa vijana uliofanyika katika kanisa la Full Gospel mjini Kilifi, Canon Kalume wa Kanisa la Anglikana (ACK) aliwahimiza viongozi wa makanisa kusimama na vijana na kusikiliza matakwa yao.

Mwakilishi wa Wanawake wa NCCK, Joyce Chigogo, aliwatia moyo vijana kujitokeza kutetea haki zao na kuwania nyadhifa za uongozi ili kulinda mustakabali wao.

“Vijana wengi hawajasajiliwa kupiga kura. Nawaomba mjisajili kwa wingi ikiwa kweli mnanuia kubadilisha nchi hii,” alisema Bi Chigogo, huku akiwasihi vijana kutotumiwa na wanasiasa wanaowapa hongo ndogo ndogo.

Mwakilishi wa Vijana wa NCCK, Lutein Kennedy Wambua kutoka Kanisa la Salvation Army, alisema Gen Z hawatachoka kudai uwajibikaji na uongozi bora. Aliwahimiza vijana kupata vitambulisho vya kitaifa na kujisajili kupiga kura kabla ya uchaguzi wa 2027.

“Miaka ya hivi karibuni, masuala ya Gen Z yamekuwa kiini cha mijadala. Kanisa lina wajibu wa kuwasikiliza na kuelewa sababu za madai yao na kuwasaidia,” alisema Canon Kalume.

Aliongeza kuwa vijana wana haki sawa ya kuongoza taifa kama Wakenya wengine na wanastahili kuungwa mkono katika harakati zao za kujumuishwa katika uongozi wa kitaifa.

NCCK pia imeikosoa serikali kwa kushindwa kutekeleza kikamilifu huduma ya afya ya kijamii (SHIF), elimu bila malipo, na kushughulikia masuala ya usalama.

Rev Kalume alisema ni jambo la kusikitisha kuwa wakuu wa shule wanapanga kufunga shule kwa sababu ya kucheleweshwa kwa mgao wa fedha na serikali. Alisema serikali ilikuwa na muda wa likizo ya Agosti kukusanya taarifa muhimu kutoka kwa shule ili kuwezesha utoaji wa fedha kwa wakati