Malalamishi na matakwa ya walimu walipokutana na Ruto Ikulu
WALIMU na wakuu wa shule walifichua changamoto kuu zinazokumba sekta ya elimu walipokutana na Rais William Ruto katika Ikulu Jumamosi wakitaka serikali iingilie kati kushughulikia ukosefu wa fedha shuleni, bima duni ya matibabu, kutopandishwa vyeo na madeni makubwa.
Mkutano huo uliandaliwa kufuatia majadiliano ya awali kati ya wizara ya elimu na vyama vya walimu, na ulikusudiwa kuangazia hali halisi ya sekta ya elimu nchini.
Mwenyekiti wa Chama cha Wakuu wa Shule za Msingi (KEPSHA), Bw Fuad Ali, alisisitiza kuwa mgao wa fedha kwa shule ni mdogo mno.
Alipendekeza kuongezwa kwa mgao wa kila mwanafunzi kutoka Sh1,420 hadi Sh2,300 ili kukidhi mahitaji ya mtaala wa CBC.
“Shule haziwezi kupata vitabu, chakula, wala kukarabati miundomsingi kwa mgao wa sasa. Tunaomba serikali iongeze pesa hizi mara moja,” alisema Bw Ali.
Pia alilalamikia kutopandishwa vyeo akisema wakuu wa shule wamesalia kwenye ngazi za chini kwa miaka mingi, licha ya majukumu mazito.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari (KESSHA), Bw Willie Kuria, alieleza kuwa shule nyingi zinadaiwa na wauzaji wa chakula, vitabu na watoaji huduma muhimu kama maji na umeme.
Alisema hali hiyo imeathiri elimu ya wanafunzi moja kwa moja.
“Kwa sasa, shule hazipokei mgao kamili. Pesa zinazotolewa hazitoshi kulisha wanafunzi, kulipia huduma, wala kutoa elimu bora. Hali ni mbaya sana,” alionya.
KESSHA pia ilipendekeza kurekebishwa kwa mfumo wa mgao, kwa kuhakikisha kila shule inapokea kiwango cha chini cha fedha kabla ya kuzingatia idadi ya wanafunzi, ili kusaidia shule ndogo zinazohangaika kujiendesha.
Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu (KNUT), Collins Oyuu, alilalamikia kutotambuliwa kwa wakuu wa shule za Sekondari Msingi wanaofanya kazi ndani ya shule za msingi.
Alisema wengi wana sifa za kitaaluma kama shahada za uzamili na uzamivu, lakini hawalipwi ipasavyo.
“Hawa walimu ni viongozi kamili wa shule. Wanastahili kutambuliwa na kupandishwa vyeo kama wenzao,” alisema Bw Oyuu.
KNUT pia ilitaka sera ya uhamisho wa lazima isitumike tena. “Walimu walitenganishwa na familia zao. Ndoa zikavunjika. Hatutaki turudi huko tena,” alisema.
Chama cha Walimu wa Sekondari na Vyuo (KUPPET) kilikosoa miongozo ya sasa ya kupandishwa vyeo, kikisema inawabagua walimu wakongwe.
KUPPET ilitaka mwongozo huo uondolewe. Akijibu malalamishi, Rais Ruto alikiri kuwa walimu wengi wamekwama kwenye vyeo vya chini kwa miongo mingi.
Alisema serikali imekuwa ikitumia Sh1 bilioni kila mwaka tangu 2023 kupandisha vyeo walimu 25,000, lakini akasema kasi hiyo ni ya chini mno.
“Tunaongeza bajeti hadi Sh2 bilioni kwa mwaka ili kupandisha walimu 50,000 kila mwaka,” alisema Rais.
Rais pia aliagiza kupitia upya miongozo ya kupandisha vyeo walimu, kuhakikisha usawa kwa walimu na watumishi wengine wa umma, na akahimiza kuharakishwa kwa utekelezaji wa mfumo wa kitaifa wa usimamizi wa elimu (KEMIS) ili kuondoa wanafunzi hewa.