Mawakili wanavyofyonza kaunti kwa huduma
Kaunti mbalimbali kote nchini zinaendelea kupoteza mabilioni ya pesa za umma kwa ada za huduma za uwakilishi wa kisheria.
Hii ni licha ya kuwepo kwa idara kamili za sheria pamoja na Ofisi ya Mwanasheria wa Kaunti ambazo zimepewa jukumu la kushughulikia masuala ya ushauri wa kisheria. Hali hii inaibua maswali mazito kuhusu uwajibikaji na matumizi mabaya ya pesa za walipa ushuru.
Wiki iliyopita, Mahakama Kuu ilitupilia mbali ombi la Serikali ya Kaunti ya Nairobi la kuzuia malipo ya Sh498.7 milioni kwa wakili mmoja kwa huduma za kisheria zilizotolewa miaka 18 iliyopita.
Uamuzi huo uliifungulia njia kaunti hiyo kulipa Bw Samson Masaba deni hili kwa huduma zilizotolewa mwaka wa 2006.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa kifedha 2023/2024 inaonyesha kuwa maafisa wa kaunti wamekuwa wakiandikisha matumizi ya kiwango cha juu mno kwa huduma za wanasheria wa kibinafsi, hata ingawa wana mawakili walio kazini.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwepo kwa mitandao ya upendeleo ambapo kampuni za sheria, nyingi zikiwa zimepewa zabuni kwa njia isiyo halali, zinaendelea kufyonza pesa za umma bila usimamizi wa kutosha, mara nyingi bila stakabadhi halali wala ushahidi wa kuhudhuria vikao mahakamani.
Katika kaunti kama Nairobi, Trans Nzoia, na Homa Bay, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu waligundua kuwa malipo ya mamilioni ya shilingi kwa huduma za sheria yalifanyika bila stakabadhi halali au mikataba ya kisheria.
Hali ya Nairobi ni ya kutia wasiwasi zaidi. Kaunti hiyo inakabiliwa na deni la kushangaza la Sh21.3 bilioni kwa ada za kisheria pekee – kiwango kinachowakilisha asilimia 11 ya madeni yote ya kaunti hiyo.
Kati ya hayo, Sh6.2 bilioni zinadaiwa na mawakili wanne pekee, sawa na asilimia 29 ya deni lote. Kaunti hiyo inakosolewa kwa kulipa ada kubwa za kisheria bila ushindani wa zabuni wala njia ya uwazi ya kuwapata wanasheria hao. Ripoti ilionyesha kuwa kati ya kesi 159, 65 pekee zilitolewa kwa mawakili wanane tu, bila sababu ya wazi jinsi walivyochaguliwa.
Hali hiyo imeenea kote nchini. Katika Kaunti ya Kilifi, kwa mfano, Sh71.5 milioni zililipwa kwa mawakili sita wa kibinafsi kama sehemu ya matumizi ya Sh276.2 milioni. Hata hivyo, wakaguzi hawakupata rekodi zozote rasmi kuhusu maagizo kwa mawakili hao, kuhudhuria mahakamani, au ushahidi kuwa ada hizo zilitozwa kulingana na sheria.
Kaunti ya Tana River nayo ililipa Sh30.7 milioni kwa kampuni nne za sheria bila idhini ya Kamati ya Utendaji ya Kaunti. Zaidi ya hayo, hapakuwa na stakabadhi za malipo hayo, ikiwemo rekodi za kesi.
Kaunti ya Mandera ilitumia Sh45.5 milioni kwa huduma za sheria bila idhini iliyoandikwa kinyume na sheria za ununuzi wa umma. Hakukuwa na maombi rasmi kutoka idara mbalimbali wala stakabadhi za kuhalalisha malipo hayo.
Katika Kaunti ya Marsabit, kaunti ililipa kampuni ya sheria Sh3.3 milioni kuwakilisha kesi ya madai ambapo mlalamishi alikuwa anadai Sh1 milioni pekee. Kaunti ilishindwa katika kesi hiyo, na gharama ikaongezeka hadi Sh4.3 milioni. Hakukuwa na ushahidi wa jinsi ada hiyo ilikadiriwa wala kufuata Kanuni za Malipo ya Wanasheria
Kaunti nyingine kama Machakos, Kisumu na Nyandarua pia ziligonga vichwa vya ripoti kwa matumizi tata ya pesa za kisheria.
Machakos ililipa Sh38.8 milioni kwa kampuni nne za sheria, lakini wakaguzi hawakupata faili zozote za kesi kuthibitisha uhalali wa malipo hayo.
Kaunti ya Kisumu, ilitumia Sh46 milioni kwa ada za kisheria bila rekodi sahihi za faili za kesi, kuhudhuria mahakamani au maelezo ya ada – hali iliyozua hofu ya ubadhirifu.
Kaunti ya Nyandarua, licha ya kuwa na maafisa watano wa sheria, ilitoa kesi 50 kati ya 155 kwa mawakili wa kibinafsi bila kufuata utaratibu wa zabuni.
Katika kaunti za Trans Nzoia, Uasin Gishu na Elgeyo Marakwet hali si tofauti.
Trans Nzoia iliteua kampuni 7 pekee kati ya 36 zilizoidhinishwa, kwa kutumia zabuni ya moja kwa moja, kinyume cha Sheria ya Ununuzi wa Umma.
Uasin Gishu, licha ya kuwa na idara ya sheria iliyo na uwezo, ilitumia Sh22.2 milioni kwa huduma za mawakili wa nje, jambo linaloibua maswali kuhusu kutotumika kwa mawakili wa ndani.
Nandi ilitumia Sh36.8 milioni bila kueleza ni kwa nini ofisi ya mwanasheria wa kaunti haikushughulikia kesi hizo.
Baringo ililipa Sh900,000 kwa huduma za kisheria bila kueleza aina ya kesi, iwapo zilikuwa Mahakama Kuu au ya Rufaa, au kutoa rekodi za kuhudhuria mahakamani.
Kaunti ya Elgeyo Marakwet ilitumia Sh2.7 milioni kwa ada za sheria bila idhini ya Kamati ya Utendaji, na bila mikataba au rekodi za kesi.
Narok ilizidisha bajeti yake ya sheria kwa Sh27.6 milioni, ikilipa Sh365 milioni dhidi ya bajeti ya Sh337 milioni bila idhini wala kufuata sheria za ununuzi.
Nakuru ilitumia Sh22.6 milioni bila kutoa ushahidi wa uteuzi wa mawakili au nyaraka kuthibitisha huduma zilizotolewa.
Kajiado ilitumia Sh79.1 milioni kwa ada za sheria bila idhini ya ununuzi, Bomet ilipoteza karibu Sh15 milioni kwa riba na adhabu, ikiwemo kesi ya ajira iliyosababisha Sh9.8 milioni za adhabu.
Kaunti ya Homa Bay ilitumia Sh53.7 milioni kwa huduma za kandarasi, zikiwemo Sh11 milioni kwa mawakili, bila kueleza ni kwa nini mawakili wa ndani hawakutumika.
Wakili wa Katiba Charles Kanjama anakubali kuwa wasiwasi kuhusu uwepo wa ufisadi katika huduma za ununuzi wa umma ni wa kweli na unafaa kushughulikiwa.