Makala

Saidia mtoto wako kukuza urafiki

Na BENSON MATHEKA September 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Mtoto wako wa shule ya chekechea anapopata rafiki mpya shuleni, uhusiano huo unaweza kuwa zaidi ya urafiki wa kawaida wa kucheza. Urafiki wa mapema unaweza kusaidia kuimarisha ujuzi wa kijamii wa mtoto wako na hata kumkinga dhidi ya matatizo ya tabia anapokua.

Kwa mujibu wa watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Illinois, urafiki wa mapema huleta manufaa mengi ya kijamii na kimaadili baadaye maishani.

Urafiki wa hali ya juu unahusisha kushirikiana, kubadilishana zamu, kushirikiana kwa upendo, na viwango vya chini vya ugomvi. Utafiti umeonyesha kuwa aina hii ya urafiki—ingawa ni muhimu kwa watoto wote—ni wa maana zaidi kwa wavulana.

Katika utafiti wa muda mrefu uliofanyika kuanzia chekechea hadi darasa la tatu, matokeo yalionyesha kuwa wavulana ambao hawakuwa na urafiki wa karibu katika chekechea, au waliokuwa na urafiki wa ubora wa kati au wa chini, walionyesha matatizo zaidi ya kitabia walipofika darasa la kwanza na la tatu.

 Kwa upande mwingine, wasichana walionekana kuwa na ujuzi mzuri wa kijamii bila kujali ubora wa urafiki wao wa mapema. Matokeo haya yalichapishwa katika  jarida la Infant and Child Development.

“Mahusiano ya rika yanazidi kuwa muhimu kwa watoto kadri wanavyokua. Chekechea hutoa fursa nyingi kwa wavulana na wasichana kujifunza jinsi ya kuhusiana na marafiki kwa njia chanya. Watoto wanapojifunza kuelewana, kusuluhisha migogoro, na kufurahia urafiki wa kweli, wanaweka msingi imara wa mahusiano mazuri ya baadaye,” asema mtaalamu wa malezi dijitali Dkt Debbie Glasser.

Je, unaweza vipi kumsaidia mtoto wako wa chekechea kuwa na urafiki wa hali ya juu? Dkt Glasser anatoa vidokezo muhimu:

Anzia nyumbani

Wewe ni mwalimu wa kwanza na mwenye ushawishi mkubwa zaidi kwa mtoto wako. Unapowasiliana kwa heshima na watu wengine—nyumbani na katika jamii—mtoto wako anajifunza kwa vitendo jinsi ya kuwatendea wengine kwa upendo, heshima, na huruma.

Chukua hatua

Kadri mtoto anavyokua, ataanza kuchagua marafiki wake mwenyewe. Lakini katika miaka ya awali, wewe una nafasi kubwa ya kuandaa michezo ya pamoja na kuwakaribisha marafiki nyumbani. Fanya juhudi za kusaidia mtoto wako kujenga urafiki katika umri huu.

Toa mwongozo

Unapowakaribisha watoto kucheza nyumbani, hakikisha uko karibu kuwasaidia kubadilishana zamu, kuelewana, na kusuluhisha tofauti kwa amani na busara. Usimlazimishe au kuingilia kila mara, bali kuwa macho na tayari kutoa ushauri pale panapohitajika.

Tafuta msaada wa ziada

 Ikiwa una wasiwasi kuhusu uwezo wa mtoto wako wa kufanya na kudumisha urafiki, au unaona changamoto katika hisia au tabia zake, usisite kutafuta ushauri kutoka kwa mtaalamu.

Urafiki wa mapema si jambo la kubahatisha unaweza kuwa msingi muhimu wa ustawi wa kijamii na kihisia kwa mtoto wako katika miaka ya baadaye