SIASA: Kumtawaza Matiang’i Jubilee Party huenda kugawanye upinzani
MPANGO wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kumpokeza Waziri wa zamani wa Usalama Fred Matiang’i uongozi wa chama cha Jubilee unafasiriwa kama ambao huenda ukaleta migawanyiko zaidi katika kambi ya Umoja wa Upinzani.
Sababu ni kwamba wandani wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, wanachukulia hatua hiyo kama inayolenga kumhujumu kisiasa kiongozi huyo wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) anayetaka kuhakikisha kuwa eneo la Mlima Kenya liko nyuma yake kuelekea 2027.
Bw Kenyatta ameitisha Kongamano Maalum la Wajumbe wa Jubilee (NDC) mwezi huu.
Mkutano huo utafanyika Ijumaa Septemba 26, katika uwanja wa Klabu ya Jockey, Ngong Racecourse, Nairobi.
Japo agenda ya kongamano hilo haijatangazwa, duru zimeiambia safu hii kwamba Bw Kenyatta atatumia fursa hiyo kumkabidhi Dkt Matiang’i uongozi wa chama hicho huku akisalia na usemi katika masuala yake japo “nyuma ya pazia.”
“Lakini Uhuru atasalia kuwa Mlezi na Mshauri Mkuu wa chama chetu tunapoelekea kukipa sura mpya na kikiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao,” anafichua afisa mmoja chama hicho aliyeomba tulibane jina lake kwa sababu yeye si msemaji wake.
Dkt Matiang’i ametangaza azma yake ya kuwania urais 2027 na anatarajiwa kutawazwa rasmi kama mgombea urais wa Jubilee katika kinyang’anyiro hicho.
Lakini wachanganuzi wanasema kuwa kwa kumtawaza rasmi Dkt Matiang’i kuwa mgombeaji urais wa Jubilee na kiongozi wake wa kitaifa, Bw Kenyatta anaonyesha wazi hana imani kwa Bw Gachagua, ambaye pia ametangaza azma ya kugombea urais 2027.
Hii ni licha ya kwamba Katiba inamzuia Bw Gachagua aliyetimuliwa afisi, kwa ukiukaji wa Katiba, Oktoba 18, 2024, kuwania kiti chochote cha kisiasa.
“Ni wazi kwamba kwa kumkabidhi Dkt Matiang’i uongozi wa Jubilee, Bw Kenyatta anaunga mkono azma yake ya urais. Bila shaka hatua hii inaonyesha kuwa hana imani na vinara wengine wa upinzani, haswa Bw Gachagua anayetoka katika ngome yake ya Mlima Kenya. Aidha, Bi Gachagua atahisi Uhuru anamkwaza kwa kumleta Matiang’i Mlima Kenya, kinyume na matakwa yake,” anasema Dan Kibe, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.
Isitoshe, hatua ya chama cha Jubilee kudhamini mgombeaji katika uchaguzi mdogo wa Mbeere Kaskazini ni kiashirio kingine kwamba chama hicho hakiungi mkomo msimamo wa upinzani kumuunga mkono mgombea mmoja ili kuzuia mwaniaji wa chama cha UDA kushinda kiti hicho.
Huku upinzani ukikubaliana kuunga mkono Newton Kariuki, almaarufu Karish, wa chama cha Democratic Party (DP) kama mgombeaji wake, Jubilee imemteua Jacob Ireri Mbao, ambaye ni kiziwi, kupeperusha bendera yake katika kinyang’anyiro hicho cha Novemba 27, 2025.
Mnamo Jumatano, Bw Gachagua alitangaza kuwa DCP imejiondoa katika uchaguzi huo na itamuunga mkono Bw Karish, ambaye ni Diwani wa Wadi ya Muminji.
Bw Gachagua alisema uamuzi huo ulitokana na hali kwamba Geoffrey Ruku aliyekuwa Mbunge wa eneo hilo kabla ya Rais William Ruto kumteua kujaza nafasi ya Muturi kama Waziri wa Utumishi wa Umma alihudumu kwa tiketi ya DP.
“Tulijadiliana na kuamua kuwa ni bora DP ipewe nafasi ya kuteua mtu atakayekamilisha miaka miwili iliyosalia kama mbunge. Pia ni kwa misingi ya kumheshimu Bw Muturi kwamba kama kiongozi mwenye ushawishi katika eneo hilo anao uwezo na sifa zitakazowezesha kupatikana kwa ushindi,” akaeleza kwenye kikao na wanahabari katika makao makuu ya DCP, Nairobi.
Mbunge huyo wa zamani wa Mathira aliongeza kuwa huo ndio msimamo wa vyama vingine vya upinzani kama vile Wiper yake Kalonzo Musyoka, People Liberation Party (PLP) yake Martha Karua na chama cha Democracy Action Party (DAP-K) kinachoongozwa na Waziri wa zamani wa Ulinzi Eugene Wamalwa.
Kulingana na Kibe, ni kinaya kwamba Jubilee imeamua kumdhamini mgombeaji ilhali mwenyekiti wake Saitoti Torome huiwakilisha katika mikutano ya Upinzani.
“Hii ina maana kuwa Dkt Matiang’i ataendesha kampeni katika jukwaa tofauti katika Mbeere Kaskazini akimnadi Bw Mbao huku akina Gachagua wakimvumisha Bw Karish. Taswira itakayojitokeza ni ya upinzani uliogawanyika, hali ambayo itavuruga nafasi yao ya kushinda kiti hicho,” anaeleza.
Mnamo Alhamisi, Dkt Matiang’i alitua mjini Embu ambako alifanya mkutano na wanachama wa Muungano wa Wataalamu wa Kaunti hiyo, ishara kwamba anajiandaa kwa kampeni katika eneo hilo.
Kuna hofu kwamba huenda kampeni za uchaguzi mdogo wa Mbeere Kaskazini ukafufua uhasama kati ya Bw Kenyatta na Bw Gachagua, huku kiongozi huyo wa DCP akihisi kuwa rais huyo mstaafu anapania kumtumia Matiang’i kumlemaza kisiasa haswa katika Mlima Kenya.