Tahariri

TAHARIRI: Rais atimize aliyoahidi walimu Ikulu

Na MHARIRI MKUU September 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MKUTANO wa Rais na walimu katika Ikulu ni ujumbe kuwa serikali bado inatambua umuhimu wa walimu kama nguzo ya elimu na maendeleo ya taifa.

Hata hivyo, ni muhimu Rais atambue kuwa walimu wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu kutimizwa kwa ahadi nyingi ambazo zimekuwa zikitolewa kila mwaka bila utekelezaji.

Sasa ni wakati wa vitendo, si maneno.

Mojawapo ya changamoto kuu zinazowakabili walimu ni kucheleweshwa kwa mgao wa fedha kwa shule, jambo ambalo linaathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za masomo na usimamizi wa shule.

Wakati serikali inatoa agizo la wanafunzi kwenda shuleni, ni lazima ihakikishe kwamba shule zina rasilmali za kutosha kuendesha shughuli zao.

Bila fedha, walimu hawawezi kufanikisha mafunzo ipasavyo, na wazazi hujikuta wakibeba mzigo wa gharama, kinyume na sera ya elimu bila malipo.

Vilevile, kupandishwa kwa vyeo kwa walimu ni suala linalohitaji kushughulikiwa kwa haraka.

Walimu wengi wamehudumu kwa miaka mingi bila kupandishwa vyeo licha ya kuwa na sifa na uzoefu unaohitajika.

Hii imesababisha hali ya kukatishwa tamaa na kupungua kwa motisha kazini.

Rais alipoahidi kushughulikia suala hili, walimu walichukulia kwa uzito, na sasa wanatarajia utekelezaji wa haraka kupitia TSC na wizara husika.

Ni lazima pia walimu walipwe marupurupu yao kwa wakati, mazingira yao ya kazi yaboreshwe, na pawepo na usawa katika uajiri na usambazaji wa walimu nchini ili kupunguza mzigo kwa walimu wa maeneo fulani.

Tunaomba Rais na serikali yake watimize ahadi hizi si kwa sababu ni shinikizo la kisiasa, bali kwa sababu ni haki.

Maendeleo ya nchi hayawezi kutimia bila walimu wenye motisha, wanaothaminiwa, na wanaopewa nyenzo za kufundisha.

Kwa kutekeleza haya, Rais atakuwa amechukua hatua ya kihistoria kurejesha heshima ya walimu, kuboresha elimu, na kuweka msingi imara wa mustakabali bora wa Kenya.