Dimba

Jepchirchir: ‘Maombi yalinisaidia kuibuka bingwa wa 42km’

Na GEOFFREY ANENE September 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

BINGWA mpya wa dunia wa marathon, Peres Jepchirchir, amefichua kuwa alitumia muda mwingi akiomba Mungu ampe nguvu na ushindi kabla ya kutwaa taji hilo mjini Tokyo, Japan, hapo Jumapili.

Jepchirchir anasema alipata motisha kutoka kwa dhahabu ya mshikilizi wa rekodi ya dunia ya 10,0000m Beatrice Chebet kwenye fani yake,  na akaamini pia ni wakati wake kufanya mambo katika marathon baada ya kuona utepe zikisalia mita 100.

“Niliona jinsi Chebet alijitahidi nikawa naomba Mungu anifanyie vile vile. Nilimwambia huu ni wakati wangu, anipe nguvu kwa ajili ya mbio. Nimefurahi kushinda medali ya pili ya Kenya,” alisema Jepchirchir, 31.

Jepchirchir akikata utepe kushinda marathon hiyo. PICHA | REUTERS

Bingwa huyo wa Olimpiki 2021 alikiri hakushiriki marathon yoyote msimu mzima kabla kuelekea jijini Tokyo, na hivyo ushindi wake ulimshangaza.

“Sikutarajia kushinda. Lakini nilipoona nimebakisha mita 100, nilianza kufyatuka na nikapata nguvu zilizojificha,” akaeleza Jepchirchir, 31.

Alionyesha pia mapenzi yake kwa Tokyo, akisisitiza kumbukumbu nzuri alizo nazo tangu kutwaa dhahabu ya Olimpiki 2021, ingawa marathon hiyo ilifanyika mjini Sapporo.

Katika fainali ya kusisimua Jumapili, Jepchirchir alishinda umbali huo wa kilomita 42 katika muda wa saa 2:24:43 – sekunde mbili mbele ya mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia, Tigst Assefa wa Ethiopia.

Wote waliingia mkondo wa mwisho uwanjani wakiwa bega kwa bega, lakini Jepchirchir aliongeza kasi katika mita 350 za mwisho akaibuka na ushindi wa pili wa Kenya kwenye Riadha za Dunia 2025.

Jepchirchir (kushoto) na Tigst Assefa wa Ethiopia bega kwa bega wakiingia katika uwanja wa kitaifa wa Japan mnamo Jumamosi. PICHA | REUTERS

Assefa, ambaye alishinda London Marathon nchini Uingereza hapo Aprili 2025, alilazimika kuridhika na fedha.

“Sipendi kusema nimepoteza dhahabu,” alisema Assef na kuongeza kuwa, “nilikuwa na changamoto katika maandalizi baada ya rekodi yangu ya London, lakini ninafuraha na medali ya fedha.”

Julia Paternain wa Uruguay alinyakua shaba kwa 2:27:23, na kuwa mwanariadha wa kwanza wa taifa lake kushinda medali ya dunia kwenye marathon.

Kenya inasalia na medali mbili za dhahabu baada ya Chebet kuanza mashindano kwa kutwaa ubingwa wa 10,000m Jumamosi.