Riadha za Dunia: Serem aondolea vidume wa Kenya aibu kwa shaba ya 3,000m kuruka viunzi na maji
EDMUND Serem amehakikisha wanaume wa Kenya hawaondoki mikono mitupu kwenye Riadha za Dunia mjini Tokyo, Japan, baada ya kung’ang’ana mita 20 za mwisho na kunyakua shaba katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji Jumatatu.
Serem alilazimika kuchomoka kutoka karibu nafasi ya saba baada ya kufungiwa katika laini ya ndani, kabla kumaliza katika nafasi ya tatu. Inamaanisha Kenya imezoa angalau medali ya mbio hizo za 3,000m SC (Steeplechase) katika makala 18 mfululizo ya Riadha za Dunia.
Aidha, medali ya Serem ni ya kwanza ya wanaume wa Kenya jijini Tokyo na ya tatu kwa jumla baada ya Beatrice Chebet na Peres Jepchirchir kutawala 10,000m na marathon mtawalia kwenye mashindano hayo ya dunia makala ya 20.

Geordie Beamish ameandikisha historia kwa kuwa raia wa kwanza wa New Zealand kutwaa taji la 3,000m SC baada ya kuibuka bingwa kwa dakika 8:33.88, mbele ya mshindi wa Olimpiki 2024 Soufiane El Bakkali (8:33.95) aliyekuwa akitetea ubingwa naye Serem akafunga tatu-bora (8:34.56).
Serem aliwapita Samuel Firewu (Ethiopia), Mmoroko Salaheddine Yazide na mshikilizi wa rekodi ya dunia Lamecha Girma wa Ethiopia waliofuatana kutoka nafasi ya nne hadi sita, mtawalia.
Kenya inaongoza jedwali la 3,000m kuruka viunzi na maji la wanaume kwenye Riadha za Dunia baada ya kuvuna dhahabu 13, fedha 12 na shaba nane tangu mashindano hayo yaanzishwe mwaka 1983. Imepata medali katika kila makala tangu 1991, ingawa dhahabu imeipiga chenga kwa makala matatu mfululizo sasa.
Kwingineko, Lilian Kasait, Catherine Amanangole, Isaac Kipkemboi na Benard Biwott wameingia Delhi Half Marathon itakayofanyika nchini India hapo Oktoba 12.