Njaa ilivyowakeketa walimu wakisubiri kupokea Sh10,000 Ikulu
WALIMU waliofika katika Ikulu ya Nairobi kwa kishindo na matarajio mengi Jumamosi walipitia changamoto tumbi nzima huku mamia yao wakisubiri kwa saa nyingi kupewa Sh10,000 kila mmoja.
Baadhi ya walimu walisikika wakilalamika kuwa pesa hizo zilikuwa ndogo mno ukilinganisha na masumbuko waliyopitia.
Baada ya kuwasili Nairobi Ijumaa jioni na wengine Jumamosi alfajiri na kukamilisha kikao cha ikulu mwendo wa saa nane mchana, baadhi ya walimu walilazimika kusubiri kwenye foleni hadi saa tatu usiku kupewa pesa zao zilizotajwa kuwa fidia ya gharama waliyotumia.
Baada ya mkutano na Rais mwendo wa saa nane, walimu waliambiwa wapange foleni wapokee ‘mlo wa mchana’. Wakapewa Sh10,000.
“Bado kuna watu wengi kwenye foleni. Siwezi kurudi Kakamega leo itabidi nilale (Jumamosi) kisha nisafiri kesho asubuhi. Sijapata thamani ya safari yangu, nimehangaika sana, hata heri nisingekuja,” akasema mwalimu mmoja aliyepewa pesa saa tatu usiku.
Alikuwa amefika Nairobi Ijumaa usiku. Mwalimu huyo alilia njaa akisema kuwa hawakuwa wamekula chochote au kunywa hata maji tangu wapewe ‘staftahi’.
Baadhi ya walimu walieleza Taifa Leo kuwa mipango yote ya kutolewa kwa hela hizo ilijaa fujo na ukosefu wa subira.
“Walikuwa wakifuata majina kulingana na alfabeti kwa hivyo nilipokea Sh10,000 saa tisa mchana. Lakini niliwaacha walimu wengi sana wakiwa wamepanga foleni,” akasema mwalimu mmoja.
Siku hiyo serikali ilitumia takribani Sh100 milioni kwa walimu, ikiwemo gharama ya kuandaa na kuratibu mkutano.
Pesa hizo zilitolewa baada ya jumla ya walimu 10,000 kuhudhuria mkutano huo ulioongozwa na Rais William Ruto, naibu wake Prof Kithure Kindiki na wakuu wa vyama vya walimu -KNUT na KUPPET.
Duru ziliarifu kuwa viongozi wa vyama vya walimu waliondoka na vitita vikubwa; kati ya Sh100,000 na Sh180,00.
Baadhi ya walimu hao walitoka maeneo ya mbali kuhudhuria mkutano huo wa kujadili jinsi ya kutatua changamoto zinazokabili sekta hiyo muhimu kwa ustawi.
Walimu waliwasili Nairobi alfajiri na kufikia saa mbili unusu za asubuhi walikuwa wameketi kwenye hema wakisubiri Rais Ruto na ujumbe wake pamoja na viongozi wa chama na miungano yao wawasili.
Wakati wa mkutano huo, heshima ya ualimu ilionekana kuisha, baadhi wakiungana na Prof Kindiki kuimba ‘faya si faya na ‘Tutam’; mirindimo ambayo sasa imepata umaarufu kwa kumpigia Rais Ruto debe achaguliwe tena mnamo 2027.
Alipokuwa akiwahutubia walimu waliotoka Nyanza, Katibu katika Wizara ya Elimu Julius Bitok alionekana kurejelea na kuivumisha Serikali Jumuishi.
Baada ya hotuba yake aliwaambia walimu wakutane ‘nyuma ya hema’ kwa ‘masuala fulani’, kauli iliyozua sherehe, walimu wakifahamu donge nono lilikuwa likiwasubiri.
Mkutano huo na walimu ulimpa Rais Ruto nafasi ya kuweka wazi hatua ambazo utawala wake umepiga katika sekta ya elimu kwa muda wa miaka mitatu.
“Tumeongeza bajeti ya elimu kutoka Sh540 bilioni hadi Sh702 bilioni, kiwango cha juu zaidi katika historia yetu. Tumeyashughulikia malalamishi ya Mtaala wa Umilisi na Utendaji (CBC) na kuwaajiri walimu 76,000. Tutaongeza idadi ya walimu ambao wameajiriwa hadi 100,000 kufikia Januari mwakani ili idadi yao iwiane na wanafunzi,” akasema Rais Ruto.
“Tumeyajenga madarasa 23,000, kuanzisha Chuo Kikuu cha Open Kenya na kuongeza ufadhili kwa wanafunzi wa vyuo vikuu pamoja na wale wa vyuo vya kiufundi,” akaongeza.
Hata hivyo, mikutano ya Rais na viongozi mbalimbali katika jamii imezua mjadala kuhusu matumizi ya ofisi na asasi za umma kuendeleza harakati zenye ajenda za kisiasa.
Naibu Gavana wa Machakos, Francis Mwangangi alisema mkutano na walimu na mingine inayoandaliwa ikulu ni kampeni tu za 2027.
“Sielewi kwa nini uwaalike walimu 10,000 ikulu, idadi ya juu ambayo itaonyesha tu kuwa unafanya kampeni. Hizo Sh10,000 ambazo walimu walipewa ni hongo tu ili wamchague Rais Ruto tena,” akasema Bw Mwangangi.