Jamvi La Siasa

Wakili: Hakuna kinachomzuia Gachagua kuwania urais iwapo nafasi za rufaa zipo

Na CECIL ODONGO, LABAAN SHABAAN September 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKILI Charles Kanjama amesema kuwa kisheria, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua anaruhusiwa kuwania urais mnamo 2027 kama kesi yake mahakamani haitakuwa imeamuliwa na kukamilishwa viwango vyote vya mahakama.

Wikendi Bw Gachagua akihutubia wafuasi Karatina, Kaunti ya Nyeri, alisema analenga kuwa rais wa Kenya 2027.

Alijishebedua kwamba kutokana na ufahamu na siasa zake ndiye mwaniaji pekee anatosha kumbandua Rais William Ruto kutoka ikulu.

Akiongea na Taifa Leo kwa njia ya simu, Bw Kanjama alisema jinsi kesi ya Bw Gachagua ipo kwa sasa, kama haitakuwa imeamuliwa hadi katika Mahakama ya Juu ifikapo 2027 basi yupo huru kuwa debeni.

“Ukweli ni kwamba kesi kuharakishwa yahitaji juhudi za mawakili na majaji na hilo halionekani katika kesi ya Bw Gachagua,” alihoji Bw Kanjama.

“Wakati mawakili walikuwa wakipambana asiondolewe mamlakani walifika hadi Mahakama ya Rufaa, lakini kesi ilirudi Mahakama Kuu walipozua maswali kuhusu jopo la majaji ambalo linastahili kusikiza kesi hiyo,” akaongeza.

Bw Gachagua alitimuliwa afisini mnamo Oktoba na Bunge pamoja na Seneti.

Kuondolewa kwake kulishinikizwa na madai ya ukabila na pia uhasama uliochipuka kati yake na Rais Ruto.

Aidha Bw Gachagua na mawakili wake walidai haki yake ilikiukwa kwa sababu mchakato wa kuondolewa kwake haukufuata sheria.

Walidai alichaguliwa na Wakenya katika uchaguzi wa 2022 na hivyo kuondolewa kwake kungejumuisha pia Rais.

Pia aliwataka majaji Eric Ogola, Frida Mugambi na Anthony Mrima ambao walikuwa wameteuliwa kusikiza kesi yake wajiondoe, akisema hawakuiamua kwa haki.

Bw Kanjama alisema jinsi ilivyo kwa sasa kesi dhidi ya Bw Gachagua inaendelea kujikokota, na kama haitakuwa imekamilishwa kufikia 2027, basi azma yake haiwezi kuzimwa.

Bw Gachagua alinukuliwa akimtaja Mbunge wa Sirisia John Waluke, ambaye aliwania ubunge licha ya kuhukumiwa kwa miaka 74, kama mfano wa kwamba yeye pia hawezi kuzuiwa kuwania cheo chochote.

“Hoja katika kesi hii si hukumu au kupatikana na hatia bali ni kutokana na nafasi ya kukata rufaa. Hii kesi ya Gachagua bado ina mategu ya jopo la majaji. Pia halengi kurejea ofisini ila anataka kuonyesha aliondolewa kwa njia haramu,” akasema wakili huyo.

Alidokeza kuwa kesi ya aliyekuwa Gavana Mike Sonko wa Nairobi iliharakishwa sababu ya njama fiche ya kumzuia asiwanie tena.

“Sonko mwenyewe alizua maswali kuhusu kesi yake na kudai majaji hawakumtendea haki huku akisema kulikuwa na nia ya kumzima asisimame ugavana,” akasema.

Kauli ya Bw Gachagua kuwa sasa atawania urais inatarajiwa kuchemsha viongozi wengine wa upinzani ambao amekuwa akishirikiana nao kumpiga vita Rais Ruto.