Habari

Serikali yaagizwa kubomoa daraja la wapita njia Thika Road

Na SAM KIPLAGAT September 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI imeamrishwa kubomoa daraja la wapita njia la Pangani kwenye barabara kuu ya Thika kwa kuingilia ardhi ya mtu binafsi ambaye hakupewa fidia.

Jopo la Kutatua mizozo ya Ardhi lilibaini kuwa kuna sehemu ya daraja hilo ambayo haikujengwa kwenye ardhi iliyotengewa Mamlaka ya Barabara Kuu Nchini (KeNHA) kwenye mradi wa barabara kuu hiyo.

Ardhi iliyoingiliwa inamilikiwa na Wakfu wa Sheikh Fazal Ilani Noordin. Aidha jopo liliamuru serikali ilipe Sh500 milioni kama fidia kutokana na sehemu ya ardhi iliyotwaliwa na barabara ya Thika.

Jopo pia lilibaini kuwa daraja hilo pia lilikuwa limezuia kufikiwa kwa ardhi hiyo na haki kwa wakfu huo ni uondolewe.

“Tumebaini kuwa daraja hilo lilijengwa kiharamu na limenyima wakfu uhuru wa kutumia ardhi yake. Sasa tumeshawishika kuwa fidia kwa sasa haitakuwa na mashiko kutokana na jinsi hali ilivyo,” akasema Mwenyekiti wa Jopo la kutatua mizozo ya ardhi Dkt Nabii Orina.

Aidha jopo hilo liliamrisha serikali ilipe Sh500 milioni kama fidia kutokana na sehemu ya ardhi iliyotwaliwa kujenga barabara ya Thika.

Serikali awali ilikuwa imependekeza fidia ya Sh53.4 milioni lakini haikuwahi kulipa hela hizo.