Habari za Kaunti

Familia yalilia haki baada ya jamaa wao kugongwa na gari la polisi Eldoret

Na TITUS OMINDE September 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

FAMILIA moja inataka haki kwa jamaa wao aliyegongwa na gari la polisi lililokuwa likiendeshwa kwa kasi katika mtaa wa Langas, viungani mwa jiji la Eldoret.

Brian Kipkosgei ambaye ni mhudumu wa pikipiki alivunjika mguu kutokana na ajali hiyo iliyohusisha gari aina ya Landcruiser likiendeshwa na polisi.

Mguu wake nusura ulemae lakini alitibiwa katika Hospitali ya Rufaa na ya Moi (MTRH) na sasa anapata nafuu nyumbani.

Familia iliahidiwa kuwa dereva husika atachukuliwa hatua za kisheria ila hilo halijatimia wamekuwa wakizungushwa tu wanapofika kituo cha polisi cha Simat.

Awali familia yake ilidai kuwa polisi wamekuwa wakijaribu kuficha ukweli kuhusu tukio hilo, na hata kuwanyima haki ya kuripoti katika kituo cha polisi kilicho karibu nao.

“Mwanangu aligongwa na gari la polisi lililokuwa likienda kwa kasi kutoka kituo cha polisi cha Langas, tangu wakti huo polisi wamekuwa wakituzuia kuripoti tukio hilo,” alsema mamake Kipkosgei, Pasiliza Kemei, ambaye pia ni mgonjwa.

Kwa usaidizi wa wakili wa Eldoret Jemutai Saurei, familia hiyo iliripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha Simat baada ya Kipkosgei kuondoka hospitalini mwishoni mwa juma.

Wakili huyo alisisitiza kuwa polisi hawana kinga dhidi ya mashtaka na kuahidi kuhakikisha taratibu zote zinafuatwa ili afisa aliyehusika afikishwe mahakamani.

“Tumekuja hapa kuripoti tukio hili tukiwa pamoja na mwathiriwa ili polisi waone majeraha ambayo gari lao lilimsababishia mteja wangu,” alisema Bi Saurei.

Ingawa hivyo, Kamanda wa Polisi Kaunti Ndogo ya Kapseret Zephaniah Kamuren amehakikishia familia hiyo kuwa uchunguzi unaendelea na watapata haki hivi karibuni.