Michezo

Police Bullets macho kwa msimu mpya baada ya kukosa tena Klabu Bingwa Afrika

Na TOTO AREGE September 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KOCHA Beldine Odemba wa Kenya Police Bullets anasema watazamia mbinu za kukuza ujasiri wa wachezaji wake chipukizi na kuboresha mashambulizi ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Wanawake Nchini (KWPL) msimu mpya unaoanza Oktoba.

Haya yanajiri baada ya Bullets kubanduliwa michuano ya kufuzu kwa kombe la Klabu Bingwa Afrika (CAF) mnamo Jumapili, walipopoteza 4-2 mikwaju ya penalti mikononi mwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ya Tanzania.

Penalti ziliamua mechi hiyo ya nusu-fainali baada ya sare ya 1-1 katika muda wa kawaida na ziada uwanjani Kasarani, Nairobi.

Bullets walipata bao la uongozi dakika ya 16 kupitia penalti ya mshambuliaji Margaret Kunihira, lakini JKT wakasawazisha kupitia kiungo Jamila Rajab.

Lydia Waganda (kulia) wa Police Bullets na Asha Mlangwa wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ya Tanzania waendea boli nusu-fainali ya mchujo wa kufuzu CAF uwanjani Kasarani, Nairobi, Jumamosi. PICHA | CHRIS OMOLLO

Ni mwaka wa pili mabingwa hao wa KWPL wameshindwa padogo kufuzu kwa Klabu Bingwa katika michuano hii ya mchujo wa klabu za kanda ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Mwaka jana wakishiriki michuano hii kwa mara ya kwanza walienda hatua moja zaidi hadi fainali lakini wakapoteza 1-0 dhidi ya Commercial Bank of Ethiopia (CBE).

“Tunataka kupalilia ukakamavu zaidi kwa wasichana hawa chipukizi ambao wengi wanacheza katika jukwaa hili kwa mara ya kwanza kabisa. Wana hamu na ari,” alisema Odemba.

“Tumepoteza mechi moja tu (katika mchujo), lakini ni hali ya soka. Tumehiari kuridhika na matokeo hayo,” akaongeza.

Kiungo Diana Ochol, 18, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya wasichana ya Butere alifurahia kushiriki mashindano hayo.

“Mechi ilikuwa nzuri na yenye ushindani zaidi kuliko za awali katika makundi. Tulipoteza kwa penalti, jambo ambalo ni la bahati nasibu. Tulitarajia kushinda ila tulipoteza nafasi nyingi za kushinda. Kila mchezo una mbinu na matokeo yake na tunajifunza kila siku,” alieleza kuhusu nusu-fainali hiyo.

Kocha Beldine Odemba wa Police Bullets katika mechi yao ya makundi dhidi ya Kampala Queens, hapo Septemba 4. PICHA | SILA KIPLAGAT

Kocha Odemba hajakata tamaa kuhusu kufuzu CAF na tayari ametupia jicho mwaka ujao akilenga kuwika ligini KWPL msimu mpya ili waingie tena mchujo kwa mwaka wa tatu mfululizo.

“Wasichana wangu wanaendelea kuimarika katika kila nyanja ya mchezo na hii itatusaidia katika ligi kwani bado lengo letu ni kurejea katika katika michuano ya kufuzu CAF mwaka ujao,” akasema.

Mabingwa hao mara mbili wa Ligi Kuu ya Kenya waliongoza Kundi A la mchujo wa CAF kwa pointi sita baada ya kufinya Kampala Queens ya Uganda 1-0 na Denden FC ya Eritrea 2-0.

Ingawa wamekosa tikiti ya CAF mwaka huu Bullets watacheza mechi ya kutafuta nambari tatu zoni ya CECAFA dhidi ya Kampala Queens uwanjani Kasarani, Jumanne.

Lorna Nyabuto (kulia) wa Police Bullets amkabili Shamusa Najjuma wa Kampala Queens mechi yao ya makundi . PICHA | SILA KIPLAGAT

Baadaye katika uwanja huo huo, JKT watashuka dimbani dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda katika fainali. Mshindi atawakilisha zoni ya CECAFA katika mechi za CAF nchini Misri mwezi Novemba.

Kocha wa JKT, Azishi Kondo, alisema wako tayari kwa kibarua cha Rayon baada ya kuzima Police Bullets.

“Tulijiandaa vizuri kwa mchezo dhidi ya Bullets. Tulitaka sana kucheza nao kwa sababu ndio wakali hapa Kenya, na tulijua tungewashinda. Sasa tunajiandaa kukabiliana na Rayon tunaamini hata wao tutawashinda kwa sababu sisi ni bora kuwaliko. Tuna ujuzi zaidi, tumejiandaa vyema na tumeazimia kushinda,” alijishasha kocha Kondo kuelekea mechi hiyo ya Jumanne.