Mng’ang’anio waanza: Jinsi chaguzi ndogo zinavyotikisa vyama na miungano
HAKUNA chama kikuu au muungano wa vyama ambao umeepuka migogoro ya ndani kabla ya chaguzi ndogo zitakazofanyika Novemba 27, mizozo ambayo inaweza kuathiri ushindi.
Viongozi wa vyama vya kisiasa wanazozana na viongozi wa ngazi za chini na makundi yanayopingana kuhusu nani atakayepeperusha bendera katika chaguzi hizo, jambo ambalo linaonyesha mgogoro unaweza kutoa mwelekeo mpya wa siasa za baadaye.
Mizozo hii inakumba karibu vyama vyote vikuu na muungano, ikiwemo chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Rais William Ruto na muungano wa Kenya Kwanza, pamoja na Orange Democratic Movement (ODM) cha Bw Raila Odinga.
Muungano wa upinzani unaoongozwa na chama cha Democracy for the Citizen’s Party (DCP) cha Rigathi Gachagua, pamoja na Wiper cha Kalonzo Musyoka, Democratic Party (DP) cha Justin Muturi, DAP-Kenya cha Eugene Wamalwa na People’s Liberation Party (PLP) cha Bi Martha Karua, ambao pia wanashirikiana na aliyekuwa Waziri wa Ndani Dkt Fred Matiang’i, unapitia changamoto za ndani.
Katika chama cha ODM cha Bw Odinga, migogoro imeibuka katika kaunti za Homa Bay, Siaya na Kakamega ambapo makundi yanapingana kuunga mkono wagombea tofauti.
Huko Homa Bay, kuna taarifa kwamba Bw Boyd Were, mwana wa aliyekuwa mbunge marehemu Ong’ondo Were, ndiye anapendelewa na chama, jambo ambalo limeanza kusababisha wanachama kuondoka.
Katika eneo bunge la Ugunja, katika chama hicho, inaonekana Bw Moses Omondi ana ushawishi mkubwa.
Wagombea wengine wanaowania kiti cha Kasipul ni mjasiriamali Philip Aroko ambaye tayari amejiuzulu chama kuwania akiwa huru, pamoja na Robert Riaga, Dkt Adel Ottoman, George Otieno aliyekuwa mwanahabari wa redio, mchambuzi wa siasa Newton Ogada na Rateng Otiende.
Katika eneo la Ugunja, mbali na Bw Omondi, kuna wagombea kama Chris Budo, wakili Maurice Okumu, mfanyabiashara Joseph Aluru, Mabw Fredrick Owino, Fredrick Oyugi Dor na Sam Okoyo.
Viongozi wa ngazi za chini Kasipul na Ugunja wamelalamikia ofisi kuu kwa kuweka wagombea bila kushauriwa, huku wengine wakitaka muafaka ili kuepuka ushindani mkali wa ndani.
Kwa hofu ya mgawanyiko zaidi, chama kimeahidi kufanya mchujo lakini bado kuna wasiwasi kwamba uteuzi unaweza kuwa wa kupendelea wawaniaji fulani.
Wakati huo huo, chama cha ODM kimepanga kuunga mkono wagombea wa UDA katika Banissa na kiti cha seneta Baringo chini ya muungano wa Kenya Kwanza.
Hata hivyo, bado kuna mgogoro Magarini ambapo ODM ilimpa tiketi ya moja kwa moja aliyekuwa mbunge Harrison Kombe, UDA ikisisitiza kuunga mkono Stanley Karisa Kenga.
Mbeere Kaskazini, chama cha DCP kililazimika kujiondoa ili kuachia chama cha DP cha Bw Muturi, baada ya mgogoro mkali wa ndani.
Dkt Matiang’i, ambaye ni mwanachama wa muungano wa upinzani, pia amejitokeza na mgombea wake katika kiti hicho, jambo ambalo limezua wasiwasi kuhusu mshikamano wa muungano.
Viongozi wa DAP-K na DCP pia wanazozozana Malava, hali inayoweza kuathiri muungano wa upinzani.