Jaji aagiza mwanajeshi aliye Uingereza akamatwe kwa kuua mwanamke Mkenya
MAHAKAMA Kuu nchini Kenya imetoa agizo la kukamatwa kwa mwanajeshi mmoja wa Uingereza na kushtakiwa kwa kuua mwanamke Mkenya, Agnes Wanjiru, huko Nanyuki, Kaunti ya Laikipia mwaka 2012.
Agizo hilo lilitolewa na Jaji Alexander Muteti kufuatia ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ambalo linaanzisha mchakato wa kumleta nchini kutoka Uingereza.
Mwanajeshi huyo anadaiwa kumuua Wanjiru katika Hoteli ya Lions Gate kati ya usiku wa Machi 31 na Aprili 1, mwaka 2012.
Jaji Muteti alisema kuna sababu za kutosha za kumkamata mshtakiwa, lakini aliagiza vyombo vya habari kutochapisha jina la mshtakiwa kwa sasa ili kulinda heshima ya mchakato wa mahakama.
DPP alisema baadhi ya mashahidi wako Uingereza lakini watapatikana mahakamani wakati wa kesi.
Licha ya uchunguzi, mshtakiwa hajajiwasilisha mwenyewe kwa maafisa wa usalama nchini Kenya, jambo lililosababisha DPP kuomba agizo la kukamatwa ili kumfikisha mahakamani.
Kesi hii inatokana na uchunguzi wa mwaka 2019 uliofikia uamuzi kuwa kifo cha Wanjiru hakikuwa cha kawaida bali ni mauaji.
Polisi wa Kenya walifanya ziara Uingereza kuhoji mashahidi na wanajeshi wa Uingereza waliokuwa wakifanya mafunzo Nanyuki.