Mahakama yashangaa kwa misingi gani DPP alimuondolea Oparanya kesi ya ufisadi
MAHAKAMA Kuu imebatilisha uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kuondoa mashtaka ya ufisadi ya Sh57 milioni dhidi ya Waziri wa Ushirika Wycliffe Oparanya, ikisema kuwa hatua hiyo haikuwa ya kikatiba.
Jaji Benson Musyoki aliamua kuwa DPP Renson Ingonga alivuka mipaka ya mamlaka kwa kupokea ushahidi mpya kutoka kwa Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) kuhusu kesi ya Bw Oparanya, kisha akaamua peke yake kufutilia mbali mashtaka hayo.
“Uamuzi wa mshtakiwa wa kwanza (DPP) kutathmini upya uamuzi wake wa kumshtaki mlalamishi wa kwanza (Bw Oparanya) haukuzingatia maslahi ya umma kwani haukuwa wa wazi, na wa kuwajibika. Sitachelea kusema kuwa mchakato huo haukuwa wa kikatiba,” alisema Jaji Musyoki.
EACC ilikuwa imependekeza mashtaka ya mgongano wa maslahi, matumizi mabaya ya ofisi, ulanguzi wa pesa na njama ya kushiriki ufisadi dhidi ya Bw Oparanya kwa madai ya kupokea Sh56.7 milioni kwa njia isiyo halali kutoka kwa serikali ya Kaunti ya Kakamega.
Awali, DPP alikubaliana na mapendekezo ya EACC lakini baadaye akabadili msimamo na kuachana na mpango wa kumshtaki Bw Oparanya baada ya kuteuliwa kuwa waziri katika serikali jumuishi.
“Tamko linatolewa kuwa uamuzi wa mshtakiwa wa kwanza (DPP) wa Julai 8 2024 wa kutathmini upya uamuzi wa kumshtaki mlalamishi wa kwanza kwa makosa ya mgongano wa maslahi, matumizi mabaya ya ofisi, ulanguzi wa pesa na njama ya kutenda kosa la ufisadi ni batili na haukuwa wa kikatiba,” alisema Jaji huyo.
Jaji Musyoki alisema kuwa ingawa kifungu cha 157(11) cha Katiba kinamlinda DPP dhidi ya kuingiliwa na mtu au mamlaka yoyote, haimaanishi kuwa ofisi ya DPP haiwezi kuchunguzwa kuhusu mienendo na maamuzi yake.
“Pale ambapo hatua au kutochukua hatua kunakiuka Katiba, wahusika hawawezi kujificha nyuma ya uhuru wa kikatiba,” alisema Jaji huyo.
Aliongeza kuwa DPP ana mwongozo rasmi kuhusu jinsi ya kutathmini maamuzi ya mashtaka na kuwa umma ulikuwa na matarajio halali kuwa DPP angezingatia mwongozo huo.
Jaji pia alisema kuwa mwongozo huo haupaswi kutumiwa kwa ubaguzi au kuchagua watu au taasisi fulani pekee.
“Madaraka aliyopewa DPP na Katiba ni ya wananchi, na DPP hutekeleza wajibu huo kwa niaba ya Wakenya. Kwa hivyo, ana wajibu wa kikatiba kueleza sababu na msingi wa maamuzi yake. Hicho ndicho kiini cha uwajibikaji,” alieleza.
Hata hivyo, Jaji Musyoki alikataa kufutilia mbali uteuzi wa Bw Oparanya kama waziri, akisema mchakato huo ulifuata sheria.
Bw Fredrick Mulaa, Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya na mashirika mengine ya utetezi walipinga hatua ya DPP wakisema kuwa haikuwa ya busara wala ya kikatiba.
Walidai kuwa Bw Oparanya hakuwa na sifa za kushikilia wadhifa huo kwa sababu alistahili kushtakiwa kabla ya uteuzi wake.
Ilikuwa imedaiwa kuwa Bw Oparanya alipokea Sh56.7 milioni kutoka kwa wakurugenzi wa kampuni za Sabema International Limited na Sesela Resources Limited.
Bw Mulaa alieleza kuwa hatua hiyo ilikuwa ya ghafla na ilinuia kumtakasa baada ya kuteuliwa kwake serikalini.