Habari za Kitaifa

Sina hofu ya kubanduliwa, ningali mwaminifu kwa utawala wa sheria, asema Faith Odhiambo

Na DAVID MUTHOKA September 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KIONGOZI wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK), Faith Odhiambo, ameelezea wazi kuwa hana hofu ya kupoteza wadhifa wake licha ya shinikizo kutoka ndani ya chama hicho.

Shinikizo hizi ziliibuka kufuatia uteuzi wake kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Serikali kuhusu fidia kwa waathirika wa maandamano, ambapo baadhi ya mawakili wameitisha mkutano wa kumng’oa madarakani kutokana na uteuzi huo uliozua mgogoro.

Wapinzani wanasema kamati hiyo inatwaa kazi inayofanywa na taasisi nyingine kama Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNCHR) na hivyo kuionya kuwa ni kinyume cha katiba.

Hata hivyo, Odhiambo anasisitiza kuwa angali mwaminifu kwa kiapo chake cha ofisi.

Katika mahojiano yake ya kina na Taifa Leo, Bi Odhiambo alielezea changamoto alizokumbana nazo na akasema azma yake ni kuwatumikia wanachama wa LSK kwa unyenyekevu na kuendelea kulinda utawala wa sheria.

“Nilikubali wadhifa huu nikijua changamoto zilizopo na mahitaji ya kuboresha chama.

Nawaambia wanachama wangu ukweli daima. Nitathminiwa kwa matendo yangu si kwa hofu au shinikizo za watu waliotaka nisiingie ofisini.

Tumepitia vizingiti vingi, hata wanakamati wamekumbwa na changamoto hizi. Lakini mimi ni mwanachama na nategemea maamuzi ya wanachama,” alisema Odhiambo.

Kuhusu madai kwamba kazi ya kamati anayowakilisha inapaswa kuwa ya Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya Kenya, Odhiambo anaeleza kuwa taasisi hizo mbili zinafanana na zinaweza kushirikiana.

“Nimefanya kazi kwa karibu na KNCHR. Tumekuwa pamoja katika maandamano, vituo vya polisi na maeneo hatari mbalimbali kuangalia matukio ya unyanyasaji dhidi ya waandamanaji,” alisema.

LSK pia imehusika katika kesi nyingi za mahakamani ikiwemo kesi za Baby Pendo na Rex Masai, ambazo zinahusiana na unyanyasaji wa polisi.