Habari za Kitaifa

Wabunge wakimbia kortini kujiunga na kesi inayotaka hazina ya CDF ifanyiwe refarenda

Na SAM KIPLAGAT September 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

BUNGE la Kitaifa limejiunga rasmi katika kesi ambayo wakili maarufu jijini Nairobi, Paul Mwangi, amewasilisha kortini akitaka mwongozo wa Mahakama Kuu, iwapo mswada wa kutaka kuingiza Hazina tatu za fedha katika Katiba unapaswa kuwasilishwa kwa wananchi kupitia kura ya maamuzi.

Jaji Chacha Mwita alikubali ombi la kutaka Bunge lishirikishwe katika kesi hiyo, na kuagiza mawakili wake kuwasilisha majibu yao ndani ya siku saba.

Bw Mwangi alielekea kortini mwezi uliopita kutafuta uamuzi wa Mahakama kuhusu iwapo Wakenya wanafaa kushiriki moja kwa moja kupitia kura ya maamuzi kuhusu hatima ya Mswada wa Marekebisho ya Katiba ya Kenya, 2025.

Mswada huo, ambao umefadhiliwa na Mbunge wa Rarieda, Otiende Amollo na mwenzake wa Ainabkoi, Samuel Chepkonga, unapendekeza kuingizwa kwa Hazina ya Maendeleo ya Maeneobunge (NGCDF), Hazina ya Usimamizi ya Seneti, na Hazina ya Kitaifa ya Uwezeshaji wa Jinsia ndani ya Katiba.

Jaji Mwita aliagiza pande zote kufika mbele yake Desemba 1, 2025, asikize hoja zao.

Mwaka jana, jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, lilitangaza kuwa Sheria ya NGCDF ni kinyume cha Katiba kwa kuvunja kanuni ya uhuru wa madaraka kati ya mihimili ya serikali.

“Sheria ya Ustawi wa Maeneobunge ya mwaka 2022 na 2023 imetangazwa kuwa si halali kikatiba.

Miradi yote chini ya NGCDF itasitishwa rasmi kufikia usiku wa manane Juni 30, 2026,” walisema Majaji Kanyi Kimondo, Mugure Thande, na Roselyn Aburili.

Baada ya uamuzi huo, Bunge liliwasilisha mswada mpya kutaka kuhalalisha upya hazina hizo kwa kuziingiza kwenye Katiba.

Wabunge walipitisha mswada huo kwa kauli moja katika Hatua ya Pili na Tatu, ambapo zaidi ya thuluthi mbili ya wabunge (wabunge 304 na kisha 298) waliunga mkono.

Mswada huo sasa umepelekwa kwa Seneti kujadiliwa na kupitishwa.

Bw Mwangi alisema endapo Seneti pia itapitisha mswada huo kwa wingi inavyohitajika, basi mswada huo utawasilishwa kwa Rais ili autie sahihi kuwa sheria.

Katika ombi lake, Bw Mwangi anasema kuwa marekebisho hayo yanabadilisha maeneobunge kuwa sehemu ya muundo wa serikali kuu, jambo ambalo linaenda kinyume na mfumo wa ugatuzi uliowekwa katika Katiba ya sasa.

Aliongeza kuwa Kifungu cha 2 cha mswada huo kinaunda Kifungu kipya cha 204A, ambacho kinabadilisha maana ya eneo bunge kuwa sio tu sehemu ya uwakilishi kidemokrasia bali pia kuwa chombo cha utawala chini ya serikali kuu.

“Hii ni kinyume na Kifungu cha 1 cha Katiba, ambacho kinasema mamlaka ya wananchi yanatekelezwa kupitia serikali kuu na serikali za kaunti pekee,” alisema.

Bw Mwangi aliongeza kuwa kuna uwezekano mkubwa mswada huu wa 2025 ukapitishwa na Seneti na kutiwa sahihi na Rais kabla ya Mahakama kutoa uamuzi wake, jambo ambalo linaweza kuwa kinyume cha utaratibu wa kikatiba.

Alisema Kifungu cha 255(1) cha Katiba kinasema kuwa, marekebisho yoyote yanayohusu masuala yaliyoorodheshwa katika kifungu hicho lazima yaidhinishwe kupitia kura ya maamuzi.

Pia, alinukuu Kifungu cha 256(5) ambacho kinasema ikiwa mswada wa marekebisho unahusu suala lililo kwenye Kifungu cha 255(1), basi Rais anapaswa kuagiza Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kufanya kura ya maamuzi kitaifa ndani ya siku 90 kabla ya kuutia sahihi.

Hata hivyo, alisema kuwa Katiba haijataja wazi ni nani anapaswa kuamua iwapo mswada unahusu masuala yaliyotajwa kwenye Kifungu cha 255(1).

“Ninaamini kuwa uamuzi wa iwapo mswada unahusu Kifungu cha 255 ni swali la tafsiri ya kikatiba, ambalo linapaswa kutolewa na Mahakama Kuu,” alisema Bw Mwangi.

Aliongeza kuwa mamlaka ya Bunge kuipatia serikali kuu jukumu la kutumia fedha kwa kazi fulani bila kujali vipaumbele vya serikali za kaunti, ni ukiukaji wa kutenganisha madaraka.

Mbali na hayo, alisema wabunge wawili waliopendekeza mswada huo walishindwa kueleza katika maelezo yao iwapo mswada huo unahusiana na masuala ya Kifungu cha 255, na kwa kufanya hivyo walikosa kuwapa Wabunge, Maseneta na wananchi nafasi ya kutoa maoni yao kuhusu tafsiri sahihi ya mswada huo.

Pia alisema Kifungu cha 204C, kinachopendekezwa katika mswada huo, kinajumuisha matumizi ya fedha za umma kwa miradi ya maendeleo ya maeneobunge hata kabla ya kugawa mapato ya serikali kuu.