Lissu agoma, ataka wanachama waruhusiwe kuingia mahakamani
MVUTANO uliibuka leo (Septemba 17,2025) kwenye Mahakama Kuu Dar es Salaam baada ya Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu kugoma kuendelea kusikiza kesi inayomwandama ya uhaini akishinikiza wafuasi wa chama chake waruhusiwe kuingia mahakamani.
Lissu alitarajiwa kutoa sababu ya pili ya pingamizi lake dhidi ya kesi hiyo, linaloegemea uhalali wa mahakama hiyo kusikilizia kesi yake.
Hatua hiyo iliwalazimisha majaji kuahirisha kusikizwa kwa kesi hiyo kwa saa nzima.
Hata wanachama wachache wa CHADEMA walioingia kwenye ukumbi wa mahakama hiyo walilazimika kutoka nje baada ya kubaini kuwa wenzao wamezuiwa.
Siku ya Jumatatu, kabla ya Lissu kupanda kizimbani, vurugu zilizuka baina ya wafuasi wa CHADEMA na polisi ambapo askari wa usalama waliwajeruhi baadhi ya wanachama hicho. Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alipotoa ufafanuzi kuhusu vurugu hizo alitahadharisha kuwa kitendo chochote cha kuwachokoza askari walio kwenye majukumu yao, kitashughulikiwa haraka.
Ufafanuzi huu hata hivyo umepokelewa na hisia tofauti tofauti huku baadhi wakihoji kuhusu uhalali wa polisi kuwapiga raia lakini wengine wameunga mkono hoja ya Muliro.
Lissu amesema hati ya mashtaka dhidi yake ina mapungufu makubwa. Anahoji ni chapisho gani hasa kuhusu matamshi yake linafaa kuwasilishwa, ama liwe kwa aina ya barua, barua pepe au chapisho jingine na kusisitiza watu wanaodaiwa kupokea taarifa hizo walipaswa kutajwa kisheria, vinginevyo hati hiyo inabaki kuwa na kasoro kubwa inayofaa kurekebishwa.