Waititu kusota jela mahakama ikikataa kufuta kifungo cha miaka 12
ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu alipata pigo baada ya Mahakama Kuu kukataa ombi lake la kubatilisha kifungo cha miaka 12 ambacho aliangushiwa na mahakama ya chini kwa kushiriki ufisadi akiwa uongozini.
Jaji Lucy Njuguna alifuta ombi la Waititu kufuatia pingamizi za Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) ambaye alidai ombi hilo halikuafikia viwango vya kusikizwa.
Waititu alikuwa akilenga kubatilisha uamuzi wa kumhukumu na kumfunga kwa msingi kuwa hakimu aliyehusika na kesi yake alikosea. Hata hivyo, jaji alikataa ombi hilo na kusema kuwa uamuzi wa kumfunga utaendelea kudumishwa wakati ambapo mchakato wa kusikiza na kuamua rufaa aliyowasilishwa unaendelea kortini.
Jaji Njuguna aliamrisha kuwa rufaa hiyo ikamilishwe ndani ya miezi minne, akionya kuwa kuendelea kucheleweshwa kwake na upande wa gavana kutasababisha kesi hiyo iondolewe.
Gavana huyo alihukumiwa mnamo Februari mwaka huu pamoja na watu wengine wanne. Walitakiwa walipe faini ya Sh53.5 milioni au wahukumiwe miaka 12 gerezani kwa kupokea hongo kutoka kwa mfanyabiashara Charles Chege Mbuthia, Mkurugenzi wa Kampuni ya Testimony Enterprise mnamo 2019.
Korti ilimpata na hatia ya kutodumisha maadili ya uongozi na kulinda mali ya umma baada ya kupokea Sh25 milioni kutoka kwa kampuni hiyo.
Alizuiwa kuwania cheo chochote cha umma kwa miaka saba. Pia alipatikana na hatia ya kuingilia utoaji tenda ya ujenzi wa barabara kwa kima cha Sh588 milioni, zabuni ambayo kaunti ilipatia kampuni hiyo hiyo Testimony.
Waititu alihudumu kama gavana wa Kiambu kati ya 2017 hadi kutimuliwa kwake na madiwani mnamo 2020 kutokana na madai ya kushiriki ufisadi.