Israeli yaanzisha operesheni ya ardhini Gaza
MAELFU ya Wapalestina waliokuwa wakiishi Gaza wamelazimika kuyakimbia makazi yao baada ya Israeli kuanzisha operesheni ya ardhini ikiapa kuuteka mji huo na kulisambaratisha kundi la Hamas.
Picha na mikanda ya video ilionyesha mamia wakikimbia na mizigo yao huku wengine wakishindwa pa kuenda.
Waziri wa Ulinzi wa Israeli, Israel Katz, aliandika katika mtandao wake wa kijamii wa X kwamba “Gaza inateketea” wakati alipokuwa akitangaza kuanza kwa operesheni hiyo ya kijeshi iliyokosolewa vikali na mataifa mbalimbali.
Mashambulio makali ya makombora yalisikika kila kona ya Gaza na vikosi vya jeshi la Israeli vilionekana kusonga mbele kwenye viunga vya mji huo.
Operesheni hiyo ya ardhini, ilitanguliwa na mashambulio mazito ya anga mnamo majuma matatu yaliyopita ambayo kwa sehemu kubwa yaliyaporomosha majengo makuba mjini humo.
Jeshi hilo lilisema limeingia katika hatua yake ya mwisho inayonuiwa kulisambaratisha kabisa kundi la wanamgambo wa Hamas.
Jeshi limesema linaamini bado maelfu ya wanamgambo wa Hamas wamejificha mjini humo.
Nalo Shirika la habari la Kipalestina la WAFA limeripoti ndege za kivita za Israeli kushambulia Gaza usiku kucha huku vifaru vya kivita vikionekana kuingia katika mji huo ambao ni makazi ya maelfu ya Wapalestina.
Awali jeshi la Israeli liliwataka wakazi kuondoka mji huo na kukimbilia katika maeneo ya kusini katika eneo la pwani lililozingirwa.
Haya yote yanatokea wakati Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Amerika, Marco Rubio akielekea Qatar kukutana na wakuu wa taifa hilo la Kiarabu, ambao bado wamekasirishwa na hatua ya Israeli kuishambulia ardhi yake na kuwauwa watu sita, akiwemo afisa mmoja wa usalama.
Akizungumza na waandishi habari alipoondoka Israeli, Rubio alithibitisha kuanza kwa operesheni hiyo ya ardhini dhidi ya Hamas.
“Kama mnavyojua Waisraeli wameanza kufanya operesheni zao huko, kwa hivyo tuna muda mfupi sana wa kufikia makubaliano,” alisema Marco Rubio.
Rubio aliyasema hayo wakati viongozi takriban 60 wa mataifa ya Kiislamu na Kiarabu waliokutana mjini Doha kwa mkutano wa dharura wa siku mbili kujadili shambulio la Israeli nchini humo kutoa wito wa kuangalia upya mahusiano yao ya kidiplomasia na taifa hilo.
Walikubaliana kwa pamoja kuchukua hatua za kisheria na kuizuia Israeli kuendelea na hujuma dhidi ya Wapalestina.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu, Ahmed Aboul Gheit, alisema ni muda sasa wa dunia kuvunja ukimya wake kuhusu ‘uchokozi’ wa Israeli.
Wakati huo huo, ripoti ya wachunguzi wa Umoja wa Mataifa imeishutumu Israeli kufanya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza ikimyooshea kidole cha lawama Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.