MAONI: Mikutano mingi ya kisiasa inashusha hadhi ya Ikulu
“UNAAMBIA marafiki zako Ikulu ni mahali patakatifu. Mimi sikuchaguliwa na wananchi wa Tanzania kupafanya kuwa pango la walanguzi. Ukisha kuwaambia hivyo marafiki zako na ndugu zako na ikashajulikana hivyo, mtu mwingine wala hakusogelei.”
Huu ndio uliokuwa usemi wa Rais wa Kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mnamo 1995 kabla ya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini humo.
Nyerere aliwashauri waliotaka kugombea Urais kuwa watu watakaoheshimu ikulu na kupafanya kuwa mahali pa hadhi isiyokuwa na mithili.
Nimeisikiliza hotuba hiyo saa mbili aliyotoa katika hoteli ya Kilimanjaro kwa waandishi wa habari baada ya kufanya ziara ng’ambo na nikavutiwa mno na msimamo wake kuhusu sifa za ikulu na wanaostahili kuwa hapo.
Kenya pia tuna fursa ya kusoma mawili matatu hivi kutoka kwa Mzee Nyerere ambaye anasalia kuwa kisima cha maarifa ya utu Afrika Mashariki. Rais Ruto ndiye mlengwa mkuu katika hadithi yangu hii fupi.
Tangu Rais achukue mikoba ya uongozi kutoka kwa mtangulizi wake Uhuru Kenyatta, amekuwa na mikutano na ujumbe kutoka sekta mbalimbali na jamii tofauti nchini.
Imekuwa sehemu ya magavana kuwapeleka wafuasi wao kuomba maendeleo katika Ikulu ya Nairobi na wengi wakapata ahadi kemkem, baadhi ni hewa na nyingine zinatimizwa.
Wanasiasa wanaendeleza uzalendo wa kikondoo kwa manufaa yao wenyewe. Wengine wanawapeleka wenzao kupokea mishiko ya fedha ziwafae kwa muda mfupi.
Tangu aingie Serikali Jumuishi, kuna ushindani mkubwa wa viongozi kufika ikulu bila kujali hoja wanazotaka Rais kuzishughulikia ama jinsi ya kuziratibu hata hizo hoja ili zikae sawasawa.
Wameanza kushindana sasa kuimba wimbo wa “tutam” kwa Rais. Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027, tutaona mambo na vijambo, aisee.
Kundi lililonitia wasiwasi ni walimu ambao ni wataalamu kupitia vyama vyao walifunga safari kuelekea ikulu.
Wakapewa Sh10,000 kila mmoja na wakacheza wimbo wa “tutam” na baadhi wakakaa kwa muda mrefu ndio wakapata fedha hizo.
Walioitwa Zebedayo walihitaji uvumilivu kwa sababu majina yaliyoanza na herufi A ndiyo yaliyoshughulikiwa awali. Walimu wakaambiwa watapewa asili mia 20 ya nyumba zote za bei nafuu.
Asilimia 10 tuliambiwa ni za wanamichezo. Je, watumishi wengine watapata asili mia ngapi? Je matatizo ya uhamisho na marupurupu kupunguzwa katika maeneo mengine ya nchi ni matatizo ya walimu ama si changamoto za maana?
Ikulu ina kazi kubwa kweli.
Paul Nabiswa ni mhariri, NTV