Habari

Tumechoka kuorodheshwa nambari moja kwa ufisadi – OCS Simon Rotich

Na KASSIM ADINASI, CHARLES WASONGA September 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SIMON Rotich, Msimamizi wa Kituo cha Polisi cha Akala (OCS), kaunti ndogo ya Gem Wagai, Kaunti ya Siaya amelalamika waziwazi mbele ya Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen mwenendo kuorodheshwa kwa Huduma ya Polisi Nchini (NPS) kama asasi fisadi zaidi nchini.

Akiongea wakati wa kikao cha Jukwaa la Usalama mjini Siaya Jumatano, Rotich alidai polisi wamekuwa wakishutumiwa kiujumla kuwa wafisadi ilhali kuna “maafisa wengi wanaohudumu kwa uadilifu.”

Afisa huyo alizishutumu kampuni za utafiti zinazoendesha kura za maoni kwa kuwaorodhesha maafisa wa polisi kama nambari moja kwa ufisadi nchini.

“Watafiti wa kampuni hizi wanapokusanya maoni kutoka kwa umma, wananchi hao huwa hawaambii kwamba nyakati zingine ni wao hupeana pesa bila kuitishwa. Hali hii imejenga dhana potovu kwamba nyakati zote ni maafisa wa polisi ambao huitisha pesa kutoka kwa raia,” akasema Bw Rotich.

Akaongeza: “Nyakati zijazo kampuni hizo zinapofanya utafiti kuhusu ufisadi, wananchi pia waorodheshwe, tumechoka kuorodheshwa kila mara kama nambari moja kwa ufisadi. Baadhi ya wananchi huleta pesa hata bila kuulizwa, baadaye wanazunguka huku na kule wakisema polisi ni wafisadi.”

Ili kuimarisha utendakazi miongoni mwa maafisa wa polisi, Rotich alimwomba Waziri Murkomen kuanzisha tuzo katika Huduma ya Polisi Nchini.

“Mheshimiwa Waziri ingekuwa bora kama serikali kupitia wizara yako ingeanzisha tuzo mbalimbali kwa maafisa wa polisi na vituo vinavyoonyesha utendakazi mzuri. Sababu ni kuwa kando na huduma hii kutajwa kama fisadi, kuna maafisa wengi na vituo vingi vya polisi vinavyotoa huduma nzuri kwa wananchi.”