Matumizi ya droni yanavyoweza kuboresha kilimo
SEKTA ya kilimo nchini Kenya inachangia karibu asilimia 22 ya pato la taifa (GDP), kwa mujibu wa takwimu za KNBS na Global Economy.com (2024).
Hata hivyo, sekta hii inahitaji mageuzi ya haraka – kutoka mbinu za jadi za kuzalisha chakula hadi mifumo ya kisasa.
Kwenye mdahalo huu, kilimo cha kisasa, kwa Kiingereza precision agriculture, kinajitokeza wazi, huku matumizi ya droni yakitajwa kama moja ya nyenzo zenye nguvu zaidi zinazoweza kusaidia kubadilisha taswira ya kilimo.

Chuo Kikuu cha Eldoret, ambacho hutoa mafunzo ya zaraa na bayoteknolojia, kimeanzisha mafunzo maalum kuhusu umuhimu wa droni katika kilimo.
Mafunzo haya yalianzishwa mwaka 2023, chuo hicho kikiwa na lengo kuhamasisha wakulima wa Kaskazini mwa Bonde la Ufa kukumbatia mifumo ya kisasa kwenye shughuli za kilimo.
“Matumizi ya droni hufanya kilimo kuwa rahisi na chenye tija zaidi,” anasema Dkt Heka Kamau, mhadhiri na Mratibu wa Kituo cha Uhamasishaji (Outreach Centre) cha chuo hicho.
Droni ina matumizi anuwai kwenye kilimo. Aidha, inatumika kufuatilia afya ya mimea, kusaidia kudhibiti wadudu na magonjwa, kupima hali ya udongo, kuratibu upandaji na unyunyiziaji dawa za wadudu na magonjwa, ikiwa ni pamoja na kufanya ramani za mashamba.

Hali kadhalika, kifaa hicho kinachopeperushwa angani sawa na ndege, kina uwezo kutoa taarifa sahihi kuhusu kiwango cha rutuba, unyevuunyevu na mahitaji ya mbolea, miongoni mwa huduma nyinginezo.
Kwa njia hii, Dkt Kamau anasema mkulima anaweza kufanya maamuzi bora badala ya kubahatisha.
Katika suala la umwagiliaji mimea na mashamba maji, droni zenye kamera maalum hutambua maeneo yenye ukame hivyo basi kuhamasisha wakulima.
“Kwa misitu, hutambua miti iliyokosa kuchipuka na vilevile kurahisisha kazi ya kuhesabu miti au kupima urefu na kipenyo chake (diameter),” anaelezea mhadhiri mtaalamu huyo.

Customized Aviation Solutions Limited (CASL), kampuni iliyoko Jijini Nairobi, inashirikiana na Chuo Kikuu cha Eldoret kutoa huduma za droni za kilimo.
Huduma za CASL, pia, zinajumuisha droni za ujenzi, filamu za anga, upimaji na uchoraji ramani kwa njia ya anga, uuzaji wa droni na kutoa ushauri.
“Unyunyiziaji mimea na mashamba dawa au fatalaiza, hutoza Sh1,000 kwa kila ekari. Droni inaweza kuhudumia ekari 70 hadi 100 kwa siku,” anadokeza Alex Mugane, Mkurugenzi wa Mauzo Customized Aviation Solutions Limited.
Hata ingawa hazijatua Kenya, baadhi ya droni zinatumika kupanda – jambo linalofaa sana kwa mashamba makubwa au maeneo magumu kufikiwa.

Mbali na kupunguza gharama ya uzalishaji na kuongeza mavuno, teknolojia hii pia inavutia vijana ambao aghalabu huona shughuli za kilimo kama kazi ngumu na ya sulubu.
Natasha Mwangi, ni mmoja wa vijana ambao ni ‘rubani’ wa droni, anayefanya kazi na Chuo Kikuu cha Eldoret.
“Matumizi ya droni yataleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo,” Natasha akaambia Akilimali kwenye ziara yetu katika chuo hicho kilichoko Kaunti ya Uasin Gishu.
Kujitolea kwake, ni ishara kuwa matumizi ya droni ni kati ya teknolojia ambazo zinavutia vijana kwenye kilimo.

Ubunifu, teknolojia na mifumo ya kidijitali inatajwa kama kivutio kikuu kwa vijana kushiriki kilimo, ikizingatiwa kuwa idadi yao kwenye zaraa ingali chini, hivyo basi kuwaundia nafasi za ajira na kusaidia kuangazia uhaba wa chakula na pia baa la njaa.
Kila mwaka, Chuo Kikuu cha Eldoret huandaa maonyesho ya kilimo-biashara ili kuhamasisha teknolojia mpya katika kilimo. Mwaka uliopita, zaidi ya wageni 18,000 walihudhuria, wengi wao wakiwa vijana ambao Dkt Kamau anakiri walioonyesha kuvutiwa sana na droni.
Kuruhusiwa kupeperusha droni, sharti uwe na kibali au leseni kutoka kwa Kenya Civil Aviation Authority (KCAA).
