Ni Maulid ya 136 mji wa kale wa Lamu wageni wakimiminika kila pembe
SHEREHE za kuadhimisha Maulid zinaendelea kuvutia idadi kubwa ya watu katika Kisiwa cha Lamu kwa shughuli nyingi tangu zilipong’oa nanga Jumatano.
Maulid ya mwaka huu ni ya awamu ya 136 tangu zilipoanza kuadhimishwa kwenye mji wa kale wa Lamu.
Kufikia Alhamisi, wenyeji na wageni waliendelea kufurika kisiwani humo, ili kushiriki tamasha hizo zinazojumuisha maombi na tumbuizo mbalimbali zinazofanyika mchana na usiku.
Mkuu wa Kituo cha Dini ya Kiislamu cha Msikiti wa Riyadha, Bw Abdallah Mohamed Abdulkadir, alisema wanatarajia zaidi ya wageni 3,000 kuhudhuria Maulid kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na kimataifa.
Msikiti wa Riyadha ndiyo kitovu cha maadhimisho ya kila mwaka ya Maulid Lamu.
Bw Abdulkadir alisema tayari wameanza kupokea wageni, wengi wao wakiwa ni waumini wa dini ya Kiislamu kutoka nchi za Tanzania, Zanzibar, Uganda, Burundi, Congo, Yemen, Oman na Uingereza.

PICHA|KALUME KAZUNGU
Maadhimisho hayo ya siku tatu mfululizo yanatarajiwa kufikia ukingoni Ijumaa usiku.
“Ninawasihi wageni na wenyeji wanaohudhuria Maulid kuzingatia kudumisha amani na umoja. Vijana waepuke dawa za kulevya na waishi kwa kuzingatia maadili. La mwisho, tukumbuke kuwaombea wenzetu wanaokabiliwa na misukosuko ya kivita na maafa huko Gaza,” akasema Bw Abdulkadir.
Maulid ni neno la Kiarabu linalomaanisha kuzaliwa. Katika muktadha wa Kiislamu, linahusu sherehe ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW).
Kwa kawaida, Maulid huadhimishwa katika mwezi wa tatu katika kalenda ya Kiislamu.
Sherehe hizi huwa na shughuli mbalimbali kulingana na tamaduni na maeneo, kama vile kusoma Qur’an na kaswida za kumsifu Mtume, hotuba kuhusu maisha, mafunzo na mfano wa Mtume Muhammad (SAW), dua, sherehe za kijamii zenye mapishi na chakula cha pamoja.

PICHA|KALUME KAZUNGU
Kufikia jana (Alhamisi), biashara pia zilinoga kisiwani Lamu kwa sababu ya idadi kubwa ya wateja wanaohudhuria Maulid.
Bw Hassan Ali, muuzaji kanzu, kofia aina ya tarbush, buibui, mitandio, hijabu na vikoi hakuficha furaha yake kwa idadi kubwa ya wateja aliopokea.
“Nimeamua kuja uwanja wa msikiti Riyadha kuuza mavazi haya ya Kiislamu. Nashukuru kwamba waumini na wageni wanaohudhuria Maulid, wote wamefika kujichukulia kanzu, kofia, buibui na vinginevyo,” akasema Bw Hassan.
Baadhi ya shughuli ambazo wageni watapata kwenye sherehe za Maulid Lamu ni densi ya Goma la Barani, Goma la Lamu, Goma la Siyu, Goma la Pate, Kirumbizi, mbio za punda, uogeleaji, ughani wa mashairi, kukariri vifungu vya Quran, mashindano ya kandanda, mbio za mashua na jahazi na kadhalika.