Habari za Kitaifa

Ni mtihani kwa UDA na ODM wakianza mchujo kabla ya chaguzi ndogo

Na WAANDISHI WETU September 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

VYAMA viwili vikuu vya kisiasa nchini – United Democratic Alliance (UDA) cha Rais William Ruto na Orange Democratic Movement (ODM) cha Raila Odinga – vimeanza maandalizi ya mchujo mkali kabla ya chaguzi ndogo za Novemba 27.

Mchujo huo unatajwa kuwa mtihani mkubwa kwa ushirikiano wa kisiasa uliozaa Serikali Jumuishi.

Vyama hivyo vinawania viti 23 vilivyo wazi kote nchini, kama sehemu ya mkakati wa kujiimarisha kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Jumamosi, Septemba 20, UDA itafanya mchujo katika Kaunti ya Baringo, eneobunge la Malava na wadi mbalimbali.

Mwenyekiti wa Bodi ya Uchaguzi ya Kitaifa ya UDA Anthony Mwaura, amesema kuwa maandalizi yamekamilika.

Magari ya kubeba vifaa vya uchaguzi yameshawasili mashinani, huku magari ya kivita yakitumwa katika maeneo yenye changamoto za kiusalama kama Baringo.

Bw Mwaura alifichua kuwa chama kimepanga kutumia takriban Sh23 milioni kuhakikisha zoezi hilo ni huru na la haki.

Kura zitapigwa kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi na moja jioni, huku matokeo yakitarajiwa kufikia saa tatu usiku.

UDA imesajili maafisa wa kusimamia kura 1,300 na makarani 1,300, ikiwa ni ishara ya umuhimu wa mchakato huo. Chama hicho kinatarajia kushinda zaidi ya asilimia 80 ya viti vinavyowaniwa.

Wakati huo huo, ODM, ambayo inaadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa, inakumbwa na mgawanyiko mkubwa.

Baraza Kuu la Kitaifa la chama hicho, chini ya uenyekiti wa Gladys Wanga, limekutana Nairobi kujadili maandalizi ya mchujo.

Hata hivyo, malalamishi ya kupendelewa kwa wagombeaji yameibua hofu ya mgawanyiko, hasa katika maeneo ya Kasipul na Ugunja.

Katika eneobunge la Kasipul, kujitokeza kwa Boyd Were, mwana wa aliyekuwa Mbunge Ong’ondo Were, kumewatishia wagombea wengine.

Baadhi wameamua kugombea kama wagombea huru. Hali kama hiyo imeshuhudiwa pia Ugunja, ambako mgombeaji anayepigiwa upatu ni Moses Omondi.

Baadhi ya viongozi wa ODM wamekashifu ofisi ya kitaifa kwa madai ya kuwalazimishia wagombeaji.

ODM imepanga kura za mchujo Kasipul Septemba 24 na Ugunja Septemba 26. Kura zitapigwa kwa njia ya moja kwa moja na kwa siri, kulingana na taarifa ya mwenyekiti wa NECC, Emily Awita.

Lakini migogoro imelazimu ODM kujiondoa Malava kufuatia mzozo kati ya Gavana Fernandes Barasa na aliyekuwa Naibu Kiongozi wa ODM, Wycliffe Oparanya.

Kwa mara ya kwanza, ODM sasa inaunga mkono mgombeaji wa UDA eneo hilo – ishara ya muafaka wa kisiasa wa viongozi hao wawili wakuu.

Muafaka huo pia unaonekana Banissa na Baringo, ambapo ODM imetangaza kutogombea, ikiachia UDA. Vilevile, UDA imekubali kutowasilisha wagombeaji Ugunja na Kasipul, ikiachia ODM.

Hata hivyo, hali ni tofauti katika Magarini, ambako ODM inasisitiza kumuunga mkono aliyekuwa mbunge Harrison Kombe, huku UDA ikimuunga Stanley Karisa Kenga. Mazungumzo ya muafaka bado yanaendelea.