Habari za Kitaifa

Polisi wapigwa darubini tena mshukiwa mwingine akifariki akiwa seli kituoni

Na HILLARY KIMUYU September 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

POLISI wanamlikwa tena baada ya mwanamume mwenye umri wa miaka 35 kufariki dunia akiwa kizuizini katika Kituo cha Polisi cha Mombasa, saa chache baada ya kukamatwa.

Kwa mujibu wa ripoti za polisi, marehemu aliyetambuliwa kama Simon Warui, alikamatwa mnamo Septemba 17, 2025, katikati mwa jiji la Mombasa na maafisa kutoka Kitengo cha Upelelezi wa Uhalifu kwa madai ya wizi, kufuatia malalamishi kutoka kwa raia.

Mashahidi waliokuwa katika kituo hicho walisema kuwa Warui alionekana mnyonge, mwenye wasiwasi na aliyefadhaika baada ya kufikishwa na kuwekwa korokoroni.

Kwa mujibu wa polisi, muda mfupi baadaye Warui aliomba kutumia choo kilichoko ndani ya seli hiyo, lakini alipokuwa huko, polisi walisikia kishindo kikubwa. Walipokimbia kuchunguza, walimkuta akiwa ameanguka sakafuni huku damu ikimtoka puani.

Alipelekwa hospitalini kwa dharura ambapo alitangazwa kuwa ameaga dunia.

Taarifa ya polisi ilieleza kuwa mwili wa marehemu umepelekwa katika  mochari kusubiri kufanyiwa upasuaji wa maiti na uchunguzi wa kina kubaini chanzo halisi cha kifo chake.

Huduma ya Polisi Nchini (NPS) ilithibitisha kuwa Mamlaka Huru ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA) imearifiwa na uchunguzi kamili utaanzishwa.

Hata hivyo, kifo cha Warui kimeibua maswali chungu nzima kutoka kwa makundi ya kutetea haki za binadamu, yakisema kuwa hali hiyo inaendeleza vifo vya washukiwa mikononi mwa maafisa wa polisi, hasa wakiwa kizuizini.

Katika miaka ya hivi karibuni, Kenya imeshuhudia ongezeko la ukatili wa polisi ikiwemo mauaji ya kiholela, utekaji nyara, mateso na vifo vya kutatanisha vya washukiwa wakiwa kizuizini.

Miezi mitatu iliyopita, tukio sawa na hili liliripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Nairobi ambapo mwalimu na bloga Albert Omondi Ojwang alifariki katika mazingira ya kutatanisha akiwa korokoroni.

Polisi walidai kuwa Ojwang alijijeruhi mwenyewe kwa kujigonga ukutani. Hata hivyo, ripoti ya upasuaji wa maiti ilibainisha kuwa alifariki kutokana na majeraha ya kupigwa kwa kifaa butu na kunyongwa.