Kesi ya ‘aliyeiba’ barua kutoka afisi ya Ruto yatupwa
Mahakama Kuu imetupilia mbali kesi iliyopinga agizo la serikali kuruhusu mashirika ya wataalamu kuthibitisha programu za vyuo vikuu, ikisema ushahidi uliotolewa ulipatikana kwa njia haramu kutoka Ofisi ya Rais.
Jaji Bahati Mwamuye aliamua kuwa mlalamishi Tom Odhiambo Ochieng hakutoa ushahidi kwamba alitumia njia za kisheria kupata barua ya ndani iliyomfanya awasilishe kesi yake. Barua hiyo ilikuwa ni mawasiliano ya ndani kati ya maafisa wakuu wa serikali, Ofisi ya Rais na Wizara ya Elimu.
“Mlalamishi hakutoa taarifa yoyote ya jinsi alivyopata barua hii. Hakuwasilisha ombi chini ya Sheria ya Kupata Habari, wala hakuthibitisha kuwa ilitolewa rasmi kwa njia halali,” alisema Jaji Mwamuye.
Jaji alibainisha kuwa mlalamishi hakuthibitisha alipata ushahidi kwa njia halali, na nakala zilizodaiwa kusambazwa hazimaanishi kuwa stakabadhi za serikali ni za umma moja kwa moja.
“Wakati alipoulizwa kuhusu uhalali wa ushahidi wake, kimya chake kinaonyesha mengi. Wajibu wa kuthibitisha kupata ushahidi halali unakuwa wa upande unaotegemea ushahidi huo, na mlalamishi hakufanikisha jukumu hili,” aliongeza.
Kesi hiyo ilihusiana na barua ya ndani iliyotolewa Mei 29, 2024, na Mkuu wa Utumishi wa Umma na Mkuu wa Wafanyakazi wa Rais kwa Katibu wa Idara ya Elimu ya Juu, Wizara ya Elimu, Kenya, Dkt Beatrice Inyangala.
Barua hiyo ilielekeza Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu (CUE) kuruhusu vyama vya wataalamu kuandaa miongozo kuhusu mafunzo ya sekta za kila moja.Hati hiyo pia ilisambazwa kwa wanachama wa Jukwaa la Ushauri na haikuwekwa kwa umma wakati wa awamu ya majadiliano.
Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor alisema ‘stakabadhi zilizopatikana kinyume cha sheria haziwezi kuwa msingi wa kuwasilisha kesi mahakamani.’Mahakama iliambiwa kuwa mlalamishi hakuthibitisha jinsi alivyopata barua hiyo na ilipatikana kinyume cha sheria.Pia, ilidai kuwa mlalamishi angeomba kupata barua hiyo kwa njia halali kama inavyoelezwa katika Kifungu cha 35 cha Katiba.
“Mambo yaliyopatikana kinyume cha sheria hayawezi kuwa msingi wa kufungua kesi,” alisema Mwanasheria Mkuu.
Katika kesi yake, Bw Ochieng alidai kuwa sera hiyo inakiuka mamlaka ya Bunge, mamlaka pekee ya CUE, na kanuni za ushiriki wa umma na utawala wa sheria.Alidai pia kuwa sera hiyo inaleta gharama tofauti kwa wanafunzi wa ndani na inawezekana kuvunja haki ya kupata elimu kwa mujibu wa katiba.
Lakini mahakama ilikubaliana na Mwanasheria Mkuu na kusema kesi ilitegemea barua iliyopatikana kinyume cha sheria na hivyo haikubaliki kama ushahidi.“Kwa kuwa ushahidi pekee katika kesi hii haukubaliki, kuendelea kuamua madai bila ushahidi halali kutakiuka kanuni ya mahakama zinafaa kuamua kesi zilizo na ushahidi halali tu.
Kwa hiyo kesi inafeli kwa msingi huu,” alisema Jaji Mwamuye.Mlalamishi alisema barua hiyo ni ya umma kwa sababu haikuwa na lebo ya “siri” na ilisambazwa kwa mashirika kadhaa ya serikali.Lakini mahakama ilikataa hoja hiyo.